Isak, kocha Howe wamenuniana
Muktasari:
- Staa huyo wa Sweden mwenye umri wa miaka 26, alianzisha mgomo huko Newcastle United ili kushinikiza uhamisho wa kwenda Liverpool na miamba hiyo ya Anfield ilifanikiwa kunasa saini yake kwa ada ya Pauni 130 milioni.
LIVERPOOL, ENGLAND: STRAIKA Alexander Isak amefichua hajazungumza na Kocha Eddie Howe tangu alipohama Newcastle United na kwenda kujiunga na Liverpool.
Staa huyo wa Sweden mwenye umri wa miaka 26, alianzisha mgomo huko Newcastle United ili kushinikiza uhamisho wa kwenda Liverpool na miamba hiyo ya Anfield ilifanikiwa kunasa saini yake kwa ada ya Pauni 130 milioni.
Howe, 47, alisema mwezi uliopita uhusiano wake na mshambuliaji Isak umebadilika baada ya mchezaji huyo kugomea kufanya mazoezi.
Straika huyo mpya wa Liverpool, Isak alizungumza katika wiki hii ya mechi za kimataifa, alipoulizwa kuhusu kuondoka kwa utata huko St. James’ Park, alisema: “Sina cha kuzungumza kwa sasa, kwa sababu hakimsaidii yeyote, si mimi wala Newcastle, hivyo tuyaache.”
Juu ya kama amezungumza na Howe na kumaliza tatizo na bosi wake huyo wa zamani, Isak kwa hasira alijibu: “Hapana.”
Isak ameanza maisha yake kwa kasi hafifu huko Liverpool, akishindwa kufunga kwenye mechi tatu alizocheza kwenye Ligi Kuu England na kushuhudia timu yake ikipoteza mechi mbili kati ya hizo, huku akitoka kapa pia kwenye mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Straika huyo mwenye kimo cha futi 6 na inchi 4 alifunga bao lake la kwanza kwenye kikosi cha Liverpool kwenye ushindi wa 2-1 katika michuano ya Kombe la Ligi dhidi ya Southampton.
Isak alifunga mabao 62 katika mechi 109 alizocheza kwa miaka miatu kwenye kikosi cha Newcastle United chenye maskani yake St James’ Park.
Labda kama timu hizo mbili mbili zitapangwa kumenyana kwenye Kombe la FA, lakini Howe na Isak hawatakutana hadi hapo Newcastle itakapokwenda Anfield, Januari 31.