Isak, Gyokeres wamponza kocha wa Sweeden
Muktasari:
- Kocha huyo wa zamani wa Blackburn Rovers amekuwa kwenye kibarua hicho cha kuinoa Sweden tangu Februari 2024, alikiongoza kikosi chenye washambuliaji kibao wenye vipaji.
STOCKHOLM, SWEDEN: SWEDEN imemfuta kazi kocha Jon Dahl Tomasson baada ya timu ya taifa kuwa na matokeo mabaya.
Kocha huyo wa zamani wa Blackburn Rovers amekuwa kwenye kibarua hicho cha kuinoa Sweden tangu Februari 2024, alikiongoza kikosi chenye washambuliaji kibao wenye vipaji.
Viktor Gyokeres na Alexander Isak, ambao walisajiliwa na Arsenal na Liverpool kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi ni washambuliaji wa kikosi hicho cha Sweden.
Sweden ipo kwenye vita ya kufuzu Kombe la Dunia 2026, lakini kipigo kutoka kwa Kosovo cha Jumanne iliyopita kimeifanya timu hiyo kushika nafasi ya pili kwenye kundi lao huku ikiwa na pointi moja tu.
Straika huyo wa zamani wa Denmark, Tomasson alikuwa kocha wa kwanza wa kigeni kuinoa Sweden, lakini kibarua chake kimefika mwisho baada ya kuiongoza timu hiyo kwenye mechi 18 na kushinda tisa.
Kocha huyo aliwashambulia mastraika wake baada ya kutoka patupu dhidi ya Kosovo, aliposema: “Sio nzuri na haya ni matokeo mabaya. Inaumiza, tumesahau namna ya kufunga na sijui kwanini.”
Lakini, Chama cha soka cha Sweden kinafahamu wazi ni nani wa kuwajibika kwenye hilo na hivyo imeamua kumfuta kazi kocha Tomasson.
Taarifa ya chama hicho ilisomeka hivi: “Chama cha Soka cha Sweden kimefikia uamuzi wa kusitisha mkataba wa Jon Dahl Tomasson kama kocha mkuu wa timu ya taifa. Uamuzi huu unatokana na matokeo mabaya kwenye mechi za kufuzu Kombe la Dunia.
“Uamuzi huo uliochukuliwa na chama cha soka Sweden umelenga kwenye timu ya taifa ya wanaume kushindwa kufanya vizuri. Bado kuna matumaini ya mechi za mchujo hivyo itachukuliwa kwa ulazima mkubwa na uwezekano wa kufuzu fainali za Kombe la Dunia.”
Kiungo wa zamani wa Arsenal, ambaye kwa sasa ni mkuu wa soka la Sweden, Kim Kallstrom aliongeza: “Tuna kundi la wachezaji ambao tunaamini tutafanya vizuri na kutengeneza mazingira ya kulifikia lengo hilo la kufuzu. Tuna imani timu itakwenda Kombe la Dunia kama tutapata nafasi ya kuingia kwenye mchujo Machi. Nachukua nafasi hii, kumshukuru Jon kwa kipindi chake (madarakani).”