Isak anunua mbwa kwa Sh96 milioni
Muktasari:
- Staa huyo wa Sweden, Isak hivi karibuni ataanza kulindwa na mbwa huyo mwenye mafunzo makubwa Doberman wakati huu akijaribu kuzoea mazingira huko Merseyside.
LIVERPOOL, ENGLAND: STRAIKA wa Liverpool, Alexander Isak ametumia Pauni 30,000 (Sh95,508,600) kununua mbwa kwa ajili ya kumlinda kutokana na kupokea meseji nyingi za vitisho vya kuawa.
Staa huyo wa Sweden, Isak hivi karibuni ataanza kulindwa na mbwa huyo mwenye mafunzo makubwa Doberman wakati huu akijaribu kuzoea mazingira huko Merseyside.
Fowadi huyo amekuwa akikumbana na meseji nyingi za kusakamwa na vitisho tangu usajili wake wa Pauni 130 milioni ulipofanyika akitokea Newcastle United na straika huyo wa umri wa miaka 26 aligoma ili kulazimisha uhamisho huo.
Isak na wachezaji wenzake kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Sweden wamekuwa wakikumbana na ujumbe wa vitisho kwenye mitandao ya kijamii kutokana na kufanya vibaya kwenye mechi za kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026.
Phoenix Dogs, imefichua mbwa huyo Doberman atakabidhiwa kwa Isak, ambaye amesaini mkataba wa miaka sita Liverpool, ambako atakuwa analipwa Pauni 300,000 kwa wiki.
Sasa Isak anaingia kwenye orodha ya wanasoka waliounua mbwa kwa ajili ya kuimarisha ulinzi kwenye makazi yao, wakiwamo pia beki wa Everton, Jake O’Brien, 24, Marcus Rashford, Kyle Walker na Jack Grealish, wote hao wakiwa na mbwa wa ulinzi makwao.