Iran yalalamika kulazimishwa kuondoka Marekani
Muktasari:
- Baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa SoFi jijini Los Angeles, mshambuliaji Mehdi Taremi amelitaka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuingilia kati na kusaidia kutatua kile alichokiita mazingira ya unyanyasaji ambayo timu hiyo imekuwa ikikumbana nayo tangu kuanza kwa mashindano hayo.
Los Angeles, Marekani. Timu ya taifa ya Iran imeibua malalamiko juu ya mazingira magumu inayokutana nayo katika fainali za Kombe la Dunia 2026, ikidai kulazimishwa kuondoka Marekani mara baada ya mchezo wake wa kwanza dhidi ya New Zealand.
Baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa SoFi jijini Los Angeles, mshambuliaji Mehdi Taremi amelitaka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuingilia kati na kusaidia kutatua kile alichokiita mazingira ya unyanyasaji ambayo timu hiyo imekuwa ikikumbana nayo tangu kuanza kwa mashindano hayo.
Kwa mujibu wa Taremi, wachezaji na benchi la ufundi walitarajia kubaki Los Angeles kwa ajili ya mazoezi ya kurejesha utimamu wa mwili kabla ya kurejea katika kambi yao ya Tijuana, Mexico, lakini walielezwa kuwa walipaswa kuondoka mara moja baada ya mchezo kumalizika.
“Hali hii si nzuri kwa maandalizi ya mechi zinazofuata. Wachezaji na benchi la ufundi wanapitia msongo mkubwa, lakini hatupati msaada wa kutosha. Tunaamini FIFA inapaswa kutusaidia zaidi,” amesema Taremi.
Mshambuliaji huyo amesema walipata nafasi ya kuzungumza na Rais wa FIFA, Gianni Infantino, ambaye alitembelea vyumba vya kubadilishia nguo vya Iran baada ya mechi, huku akiahidi kufanya kila linalowezekana kusaidia baadhi ya maofisa wa Iran ambao hawakupata viza kuingia Marekani ili waweze kuhudhuria michezo iliyosalia ya hatua ya makundi.
Kocha Amir Ghalenoei naye ameeleza kutoridhishwa kwake na mpangilio huo, akisema timu hiyo ilikuwa imepanga kuwasili siku mbili kabla ya mechi lakini haikuruhusiwa kufanya hivyo, na hata mpango wa kubaki Los Angeles hadi siku iliyofuata ulipingwa bila maelezo yoyote.
“Inaonekana kuna watu wengine wanaotupangia mambo. Hatuelewi kwa nini tunarudishwa Tijuana. Kwa kweli ni jambo la kushangaza na linaathiri maandalizi yetu,” amesema Ghalenoei, akiongeza kuwa Iran ndiyo timu inayokumbana na mazingira magumu zaidi katika mashindano hayo.
Tangu kuzuka kwa mvutano wa kisiasa kati ya Iran na Marekani mwezi Februari, ushiriki wa taifa hilo katika Kombe la Dunia umekuwa ukikabiliwa na changamoto.
Rais wa Marekani, Donald Trump, amewahi kuonya kuhusu usalama wa raia wa Iran, huku timu hiyo ikihamisha kambi yake kutoka Arizona, Marekani kwenda Mexico na baadhi ya wajumbe wake kukosa vibali vya kuingia Marekani.
Iran ilisafiri hadi Los Angeles siku moja kabla ya mchezo dhidi ya New Zealand, huku baadhi ya wachezaji wakidai walikumbana na ucheleweshaji mpakani. Licha ya changamoto hizo, Taremi amesema timu hiyo itaendelea kupambana kwa ajili ya kushinda michezo yake miwili iliyosalia dhidi ya Ubelgiji na Misri.