Inter Milan ilivyogeuza maumivu kukosa 'treble' ikibeba ubingwa Serie A 2025/26
Muktasari:
- Timu hiyo iliifunga Parma mabao 2-0, Jumapili, na kufanya taji la Serie A kurejea Milan na sasa iko mbele kwa pointi 12 dhidi ya Napoli iliyopo katika nafasi ya pili huku zikiwa zimesalia mechi tatu kumalizika kwa mashindano hayo.
MILAN, ITALIA: INTER Milan, juzi ibeba ubingwa wa Ligi Kuu Italia (Serie A), ikitoka kugeuza maumivu ya kukosa treble (yaani mataji matatu makubwa ndani ya msimu mmoja), msimu uliopita na kufanya mambo makubwa huu ingawa imeishia njiani Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Timu hiyo iliifunga Parma mabao 2-0, Jumapili, na kufanya taji la Serie A kurejea Milan na sasa iko mbele kwa pointi 12 dhidi ya Napoli iliyopo katika nafasi ya pili huku zikiwa zimesalia mechi tatu kumalizika kwa mashindano hayo.
Kufikia Mei 2026, Inter Milan imeshinda mataji 21 ya Serie A (Scudetti), kulingana na ripoti za Transfermarkt na Yahoo Sports. Taji lao la karibuni ndo hilo la msimu huu, likiimarisha na iko nafasi ya pili kwa klabu zenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya Italia nyuma ya Juventus iliyobeba mara 36, huku AC Milan ikiwa na 19.
Inter inaweza kubeba mataji ya ligi (FA) na Kombe la Italia ikiwa itaifunga Lazio katika fainali inayotarajiwa kupigwa Mei 13, mwaka huu ambapo mara ya mwisho iliposhinda yote mawili ilikuwa chini ya Kocha Jose Mourinho 2010 alipoiwezesha kushinda treble.
Hii ni tofauti kubwa na maumivu ya mwaka jana ambapo msimu uliokuwa na matumaini makubwa uliiacha timu hiyo bila taji lolote. Ikiwa imebakiza zaidi ya mwezi mmoja kumalizika kwa msimu uliopita, Inter ilikuwa njiani kushinda treble, lakini ilimaliza pointi moja nyuma ya bingwa wa Serie A, Napoli, na ilitolewa nusu fainali ya Kombe la Italia kisha ilichapwa mabao 5-0 na Paris Saint-Germain katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya yenye tofauti kubwa zaidi katika historia. Hapa chini ni sababu zilizoifanya Inter kubadilika na kushinda ligi ya Italia msimu huu
MABADILIKO YA KOCHA
Haikushangaza sana pale Kocha Simone Inzaghi alipoondoka Inter Milan mwishoni mwa msimu uliopita, lakini uteuzi wa Cristian Chivu uliibua maswali kutokana na uzoefu wake mdogo katika timu kubwa, hasa katika mbio za kuhakikisha kwamba timu inakimbizana vilivyo na ubingwa.
Chivu alitumia kwa mafanikio makubwa mfumo wa 3-5-2 unaotilia mkazo umiliki wa mpira wa kushambulia kwa kasi kuelekea mbele, presha ya kurejesha mpira mara tu unapopotea (gegenpressing), na matumizi ya nguvu na kasi ya wing-back.
Kocha huyo pia aliboresha mfumo uliokuwa unatumiwa awali na mtangulizi wake, Inzaghi wa kumtumia Yann Bisseck kuimarisha uthabiti wa safu ya ulinzi, huku akimpa Federico Dimarco jukumu la kuongoza mashambulizi ya ziada upande wa mbele. Kuingizwa kwa Bisseck kama chaguo la mara kwa mara la kubadilishana na Benjamin Pavard kulileta unyumbufu zaidi na kuboresha ulinzi.
Inzaghi aliondoka akiwa ameinoa Inter kwa miaka minne, akiiwezesha kushinda ubingwa wa Serie A 2024 na kufika fainali mbili za Ligi ya Mabingwa. Pia alishinda Kombe la Italia mara mbili akiwa na timu hiyo.
Chivu anakumbukwa kwa kuiongoza mechi 13 za Serie A, akiisaidia Parma kubaki Ligi Kuu Italia ikiwa ni kazi yake ya kwanza ya ukocha wa timu kubwa Februari. Lakini aliifahamu vyema Inter, baada ya kutumia miaka saba kuzinoa timu za vijana za klabu hiyo, ambako pia alimalizia soka lake enzi akicheza mwaka 2014.
Beki huyo wa zamani wa kimataifa wa Romania alikuwa sehemu ya kikosi cha Inter kilichoshinda treble 2010, akinyanyua mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Serie A na Kombe la Italia. Pia aliisaidia Inter kushinda mataji mengine mawili ya Serie A kati ya tisa aliyoshinda katika miaka saba klabuni hapo. Mbinu mpya za Chivu na mawazo mapya yaliipa Inter Milan nguvu mpya. Aliibadilisha timu kuwa ya kushambulia zaidi na kutia presha ya juu kwa wapinzani, huku akirejesha maelewano ndani ya kikosi na kuwajumuisha vijana wa akademi kama Pio Esposit
Safu ya kiungo inafanya kazi kwa kubadilika kulingana na hali ya mchezo, mara nyingi mchezaji mmoja akishuka kusaidia ulinzi wakati wa kujenga mashambulizi huku mabeki wakisogea mbele. Ushirikiano kati ya Lautaro Martínez na Marcus Thuram ni muhimu katika safu ya ushambuliaji, wakibadilishana nafasi na mmoja akishuka chini kupokea mpira mwingine hufanya mikibio zaidi ya mbele.
Timu hiyo pia inaweka mkazo kwenye presha ya juu na ya haraka. Wanapopoteza mpira, wachezaji hasa wing-back husogea mbele mara moja, kulazimisha makosa kwa wapinzani na kurejesha mpira haraka katika maeneo yao.
MAJERAHA KWA WAPINZANI WAO
Chivu alianzisha mbinu mpya za mazoezi ili kuboresha utimamu wa wachezaji, ambapo wachezaji walipiga tizi la kishkaji lakini likiwa ni la uhakika. Majeraha yaligharimu Inter msimu wa 2024-25, lakini mbali na Denzel Dumfries na Hakan Çalhanoglu, wachezaji wengine muhimu waliweza kuepuka kukaa nje kwa muda mrefu.
Nahodha Lautaro Martínez alikosa mechi nane kati ya tisa za mwisho kabla ya kurejea dhidi ya Parma. Hali hiyo ilikuwa tofauti kwa wapinzani wao, hasa Napoli. Mabingwa watetezi wangeweza kutoa ushindani mkubwa zaidi kama siyo majeraha yaliyowakumba wachezaji wa Antonio Conte msimu mzima.
Matatizo kwa majeraha Napoli yalianza hata kabla ya msimu kuanza, mshambuliaji nyota Romelu Lukaku alipokosa miezi kadhaa. Kevin De Bruyne na Frank Anguissa pia walipata majeraha ya muda mrefu, huku David Neres, Billy Gilmour na Amir Rrahmani wakikosa mechi nyingi.
KUREJEA BAADA YA KUYUMBA
Wakati fulani, msimu wa Inter Milan ulionekana kuporomoka tena kama mwaka uliopita na ilitolewa na Bodo/Glimt katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini ilijibu kwa kuifunga Genoa na kujitengenezea pengo la pointi 13 katika Ligi Kuu Italia (Serie A).
Hata hivyo, huo ulikuwa ushindi mmoja kati ya miwili katika mechi nane za ligi, ikiwemo kupoteza Dabi ya Milan dhidi ya wapinzani wao wakubwa, Inter Milan. Hali hiyo ilipunguza pengo hadi pointi sita, huku nusu fainali ya Kombe la Italia dhidi ya Como ikiwa bado wazi baada ya suluhu katika mchezo wa kwanza.
Inter ilimaliza kipindi hicho kibaya kwa ushindi wa mabao 5-3 dhidi ya AS Roma na tangu hapo haikuangalia nyuma, ikiimarisha uongozi wake na kushinda dhidi ya Como kufuzu fainali ya Kombe la Italia.