Ile vita ya Amorim, Slot inaendelea England
Muktasari:
- Slot alirusha kijembe kabla ya chama lake la Liverpool kumenyana na Brentford, kwamba atakwenda kukabiliana na timu inayocheza staili ileile ya mipira mirefu, akiilenga Man United.
LONDON, ENGLAND; KUMEANZA kuchangamka. Ndicho unachoweza kusema baada ya kocha wa Manchester United, Ruben Amorim kuingia kwenye vita ya maneno na mwenzake wa Liverpool, Arne Slot kufuatia kauli yake ya kuponda staili ya uchezaji ya miamba hiyo ya Old Trafford.
Slot alirusha kijembe kabla ya chama lake la Liverpool kumenyana na Brentford, kwamba atakwenda kukabiliana na timu inayocheza staili ileile ya mipira mirefu, akiilenga Man United.
Slot amesema: “Tulipokuwa na mapumziko, niliangalia ni mipira mirefu kiasi gani tulilazimika kukabiliana nayo, ilikuwa 178 katika mechi saba.
“Man United walipokuja, tulikabiliana na mipira mirefu 59. Lazima tujipange.”
Hicho kilikuwa kijembe cha pili cha Slot kwa kocha Amorim tangu aliposhuhudia timu yake ya Liverpool ikichapwa 2-1 na Man United uwanjani Anfield, ambapo Mashetani Wekundu walicheza mipira mirefu mingi ikitoka kwa kipa wao, Senne Lammens.
Alipozungumza baada ya mechi, Mdachi huyo amesema: “Siku zote ni ngumu sana kucheza na timu inayokabia chini na inayocheza mipira mirefu.”
Lakini, Amorim, ambaye kikosi chake kilikabiliana na Brighton uwanjani Old Trafford, Jumamosi, hakufurahishwa na kauli hiyo na kuamua kujibu: “Sijali kitu anachosema Slot. Wakati mwingine tunahitaji kuelewa mazingira ya mchezo. Nafurahia timu yangu inaweza kucheza aina tofauti ya mchezo. Hivyo, sihitaji mtu yeyote afanye uchambuzi wa timu yangu. Naweza kuichambua mwenyewe.
“Ulikuwa ushindi muhimu, lakini nilikuwa wa kwanza pia niliyesema tunahitaji kucheza vizuri tukiwa na mpira. Liverpool ilishapita, sio muhimu tena.”
Kocha wa Newcastle United, Eddie Howe hakutaka kujibu kijembe cha Slot alipodai kwamba Newcastle ni klabu ndogo. Hiyo alikuwa na maana jinsi Newcastle United ilivyolishughulikia suala la mshambuliaji Alexander Isak kwenye mpango wake wa kuhamia Liverpool.
Slot aliipiga kijembe Newcastle baada ya straika Isak, iliyemuuza kwa Pauni 130 milioni kwenda Anfield kugomea kwenda pre-season na timu hiyo na kuamua kufanya mazoezi kivyake katika kipindi alichokuwa akilazimisha uhamisho wake ili akakipige Liverpool.
Baada ya ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Eintracht Frankfurt, Slot amesema: “Huwezi kumlinganisha mchezaji ambaye hakufanya mazoezi au pre-season kwenye klabu ndogo.”
Alipoulizwa kuhusu maneno hayo ya Slot, Howe amesema: “Alex sio tena mchezaji wa klabu hii, hivyo siwezi kusema chochote.”