Ian Wright: Ona Mainoo anavyomtia aibu Amorim
Muktasari:
- Gwiji wa Arsenal, Ian Wright, alisema kufufuka kwa Mainoo kunapaswa kumfanya Amorim ajisikie aibu kutokana na namna alivyomtendea kiungo huyo katika wakati wake huko Old Trafford.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA, Ruben Amorim amekosolewa vikali kufuatia kurejea kwa kiwango cha juu kwa kiungo chipukizi wa Manchester United, Kobbie Mainoo, chini ya uongozi wa Michael Carrick.
Gwiji wa Arsenal, Ian Wright, alisema kufufuka kwa Mainoo kunapaswa kumfanya Amorim ajisikie aibu kutokana na namna alivyomtendea kiungo huyo katika wakati wake huko Old Trafford.
Lakini, tangu Carrick alipoteuliwa kuwa kocha wa mpito mwezi uliopita, mchezaji huyo aliyepitia akademi ya klabu amekuwa nguzo muhimu katika kurejea kwa mafanikio kwa Man United. Ushindi wa Man United wa mabao 2-0 dhidi ya Tottenham Hotspur, ulikuwa ushindi wao wa nne mfululizo chini ya Carrick.
Mainoo amecheza karibu kila dakika katika ushindi dhidi ya Man City, Arsenal, Fulham na Spurs. Matokeo hayo yameipandisha Man United hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa EPL.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 alikuwa anafikiria kuondoka kwenye dirisha la Januari alipokuwa chini ya Amorim, huku Napoli wakionesha nia ya kumsajili. Lakini, kufutwa kazi kwa Amorim kumegeuza kabisa hatima ya Mainoo klabuni.
Tayari ametoa asisti mbili za mabao na amekuwa na mchango mkubwa katika safu ya kiungo wakati wa msururu wa ushindi wa hivi karibuni. Akizungumza kwenye kipindi cha Premier League World Show, Wright hakuficha hisia zake, aliposema: “Kila mtu alikuwa amechanganyikiwa na kile kilichokuwa kinaendelea chini ya Ruben Amorim. Unaangalia mchezaji wa akademi ya Man United ambaye hapati nafasi, akiwa karibu sana kuondoka klabuni. Hilo ni jambo la kuaibisha sana kwa Ruben Amorim, kwa kusema ukweli kabisa.”
Wright aliongeza kuwa Carrick amewapa wachezaji uhuru wa kujieleza uwanjani, jambo ambalo Mainoo amelifaidi sana. Mfumo wa Amorim wa 3-4-3 ulimwacha Mainoo nje ya kikosi, huku Casemiro na Bruno Fernandes wakipewa nafasi katikati.
Carrick amebadili mfumo hadi 4-2-3-1, akimfanya Mainoo kucheza sambamba na Casemiro. Baada ya ushindi dhidi ya Spurs, Carrick alimsifu Mainoo kwa ukomavu wake, alisema : “Hakuna shaka kuhusu uwezo wa Kobbie na kile anachoweza kuiletea timu. Bado ni kijana sana na anaendelea kujifunza mchezo, hata kama watu wengi wanasahau hilo.”