Huyu ndio Pochettino sasa

LONDON, ENGLAND. TETESI za Mauricio Pochettino kujiunga na Chelsea zimezidi kupamba moto huku baadhi ya ripoti zinadai kwamba kila kitu kipo sawa na kinachosubiriwa ni utambulisho wake tu.

Pochettino ambaye amekuwa nja ya uwanja tangu aachane na PSG mwaka.. atajiunga na Chelsea kuchukua mikona ya Frank Lampard ambaye anahudumu kama kocha wa muda wa timu hiyo.

Lakini kila kocha huwa na tabia na mbinu zake ambazo wachezaji wa timu husika watatakiwa kujiandaa nazo. Hizi hapa ni tabia na mambo ambayo Pochettino huwa nayo ama huyafanya awapo kwenye timu.


HAKOSI NDIMU OFISINI KWAKE
Ukienda kwenye ofisi ya Pochettino lazima utakutana na trei lililojaa ndimu hiyo ni kwa sababu mmoja ya marafiki zake aliwahi kumwambia kwamba tunda hilo linapunguza hali ya hasira, mawazo mabaya na uchovu.
Akizungumza na tovuti ya talkSPORT mwaka 2019 Pochettino alisema :"Ndimu zipo ofisini kwangu ili zipunguze hali ya uchovu na kujisikia vibaya kwa wachezaji ama benchi la ufundi, kuna watu huwa wanakuja mazoezini na hali mbaya ya kimawazo, tunda hilo huwa kama tiba, wakitumia hurudi kwenye hali yao ya kawaida, huwa nayabadilisha kila baada ya siku 10 ama tatu muda mwingine itategemea na hali yake."


TEKNELOJIA SIO SANA
Licha ya uwezo wake mkubwa wa kutumia vifaa vya kisasa, Pochettino  pia hupendelea kutumia njia ya kizamani ya kuandika kila kitu kwenye kidaftari chake kwa kushuhudia mwenyewe kwa macho yake.
Akiandika kwenye kitabu chake cha Brave New World, anasema: "Ninahitaji taarifa na majaribio ya kisasa ili kuchambua lakini kitu ambacho huwa nakizingatia zaidi ni jinsi miili yao inavyofanya kazi kwa kuwaangalia kwa macho ya kawaida, nikifanya hivyo huwa najua ni kwa namba gani wanapambana na nini kifanyike"


KUPITA JUU YA MAKAA YA MOTO
Katika miaka yake mitano akiwa na  Spurs, Pochettino alifanikiwa kuiwezesha timu hiyo kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2019 ambapo walicheza na Liverpool.
Wakati wanajiandaa kwenda kwenye mechi hii, wachezaji na bencbi la ufundo la timu hiyo walitembea kwenye makaa ya mawe ya moto.
Alipoulizwa Pochettino kuhusiana na suala hili alisema:" Wote kwa pamoja waliungana na walifurahia."


MBIO TU
Anajulikana sana kwa tabia yake ya kupenda wachezaji kukimbia sana wawapo mazoezini ili kujenga uwezo wa kuwa na kasi na kutokata pumzo pale wawapo uwanjani.
Kumekuwa na njia moja ya ukimbiaji iitwayo Gacon test ambayo ndio amekuwa akiitumia sana kwenye mazoezi ya timu zote alizocheza.
Kwenye kitabu chake Pochettino ameelezea jinsi njia hiyo inavyofanya kazi akisema kwamba:"kwa kuanzia wachezaji huwa na sekunde 45 za kukimbia mita 150 kisha wanapumzika kwa sekunde 15 kisha watatakiwa kukimbia tena mita 6.25 kwa kasi zaidi.

SABUNI ANACHAGUA YEYE
Wachezaji wa Chelsea watatakiwa wawe makini na aina ya sabuni ambazo wananunua kwenye maduka mbali mbali kwani kocha huyu huchagua sabuni ya aina moja ambayo ndio huhitaji iwe inatumika kusafishia jezi na vifaa vya timu ya kwanza anayoifundisha.
Kwake yeye harufu ya jezi ni kitu anachokizingatia haswa kwenye mechi.

ANA REKODI KILA KITU
Mchezaji wa zamani wa Tottenham Danny Rose anasema kwamba Pochettino ndio kocha wa kwanza kumshuhudia akirekodi kila kitu kwenye mazoezi hadi mechi, hakuna atakachoacha hata pale watakapoenda Gym.
Akizungumza na The Telegraph, Rose alisema: "Ana rekodi hadi mazoezi, ni kocha wa kwanza kumshuhudia akirekodi mazoezi, hakuna kitu utakachomficha, kuna siku tulicheza na  Crystal Palace, nilifikiria kuwa nimecheza vizuri, kesho yake akaniita ofisini kwake ili kuchambua nilivyocheza, nilidhani kwamba angenionyesha video zangu nzuri za mchezo huo lakini ajabu kulikuwa na video 26 za makosa niliyoyafanya."


HAPIGI FAINI
Tofauti na makocha wengine, Pochettino ni mpole sana linapokuja suala la  kuadhibu wachezaji wake kwa kuwapiga faini ama kuwasimamisha.
Yeye anaamini kwamba wachezaji ni watu wazima hivyo wanaheshimiana wao kwa wao ingawa kuna baadhi ya taratibu ambazo huziingiza kwenye timu ikiwa ni katika harakati za kujenga umoja.
Mwaka 2016 alipofanyiwa mahojiani alisema kwamba:"Hapo awali nilikuwa na sheria sheria nyingi lakini kwa sasa nimezipunguza kwa sababu naamini wanaheshimiana kuanzia ndani na nje ya uwanja, sheria hizi zilizokuwepo zamani zimekuwa tabia, kwa mfano ilikuwa ni lazima asubuhi wachezaji wanapokutana mazoezini au wanapokuwa hotelini lazima wasilimiane kwa kushikana mikono na kusema 'hello', hiki ni kitu kidogo lakini kinajenga umoja sana kwenye timu.