Kane amvuka Erling Haaland
Muktasari:
- Ushindi huo ulikuwa mkubwa wakwanza kwa Vincent Kompany tangu achukue mikoba ya kuinoa Bayern msimu huu.
MUNICH, UJERUMANI: STAA wa Bayern Munich, Harry Kane ameivunja rekodi ya Erling Haaland baada ya kufunga hat-trick kwenye ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Holstein Kiel katika Ligi Kuu Ujerumani.
Ushindi huo ulikuwa mkubwa wakwanza kwa Vincent Kompany tangu achukue mikoba ya kuinoa Bayern msimu huu.
Kane alipiga hat-trick na kutoa pasi ya bao akikamilisha hat-trick yake dakika ya 91 kwa mkwaju wa penalti.
Hata hivyo, wakati mechi hiyo inaenda mapumziko Kane tayari alishaandika rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kuhusika katika mabao 50 ya Bundesliga kwa haraka zaidi akifanya hivyo katika mechi 35.
Rekodi hiyo inajumuisha mabao aliyofunga na asisti alizotoa ambapo kabla ya mchezo huo alikuwa tayari amehusika katika mabao 47 kwenye mechi 34.
Rekodi hiyo aliifikia ndani ya dakika 45 tu za kipindi cha kwanza ambapo alifunga mabao mawili na kutoa pasi moja ya bao kabla ya kipindi chapili kuongeza bao lingine lililofanya idadi iwe 51.
Hiyo imemfanya kuivunja rekodi ya Haaland ambaye alifikisha idadi hiyo kwa mjumuisho wa mabao na asisti baada ya mechi 42.
Kijumla Kane amefunga mabao 39 na asisti 11, katika mechi 35 na mashabiki wa Bayern watakuwa wanaangazia kuona staa huyo akihamishia kasi hiyo ya utupiaji kwenye michuano ya kimataifa ambapo kesho watakuwa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Dinamo Zagreb.