Huu ni mwisho wa Mo' Salah Liverpool?

LIVERPOOL, ENGLAND. TAARIFA za kuondoka kwa mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah zimeibuka kwa kasi ghafla tu kutokana na kile kilichotokea katika mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya West Ham ambao ulimalizika kwa sare ya 2-2.

Salah alionekana akitupiana maneno na kocha wake Jurgen Klopp wakati akisubiri kuingia uwanjani akitokea benchini.

Wawili walikuwa pamoja kwenye kikosi cha majogoo na kushinda mataji mbalimbali kwa miaka mingi lakini katika siku za hivi karibuni mambo hayaonekani kuwa mazuri kati yao.

Wakati wawili hao wanatupiana maneno, Darwin Nunez alisimama katikati na kumzuia Salah alimsogelee Klopp na baada ya tukio hilo kocha huyo alisema walishayamaliza kwenye vyumba vya kubadilishia nguo huku Salah alipoulizwa alisema akiongea moto utawaka.

Jambo hili linazuka wakati msimu ukiwa unaenda ukingoni huku bado tetesi zikidai Waarabu kutoka Saudia wanahitaji huduma ya mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Misri na wapo tayari kutoa Pauni 150 milioni kama mshahara kwa miaka mitatu.

Waliwahi kufanya hivyo katika dirisha lililopita lakini Salah alikataa na kusisitiza anahitaji kuendelea kubaki Liverpool.

Lakini kwa kilichotokea inaonekana hana furaha na wataalam wa mambo wanadai itakuwa ngumu tena kumbakisha.

Wachezaji wa zamani na wachambuzi baadhi walitolea maoni kilichotokea kati yake na Klopp, wengine wakisimama naye na wengine wakimkosoa.

Mchezaji wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher alisema mambo kama yale yanatokea baada ya mchezaji kujiandaa kwa muda mrefu ili kuingia uwanjani jambo linalompa hasira kocha. Hivyo Salah ndio ana kosa.

Pia mchezaji mwingine mstaafu wa timu hiyo, Peter Crouch, alisema kilichotokea sio kizuri kwa timu na huenda Salah alikasirika kwa kuwekwa benchi.

"Sijui walichokuwa wanaongea lakini kwa kutazama tu hakuna usalama pale, Mo Salah ni mchezaji aliyecheza mechi nyingu za Liverpool lazima atakuwa na hasira kwa kuwekwa benchi."