Howe atoa msimamo kwa Isak, saa zikizidi kukatika
Muktasari:
- Kocha huyo alikiri kuwa hawezi kusubiri hadi Jumatatu saa 6:59 usiku dirisha la usajili litakapofungwa, hivyo uamuzi unaweza ukatoka mapema leo.
NEWCASTLE, ENGLAND: KOCHA wa Newcastle United, Eddie Howe bado hana uhakika juu ya mustakabali wa straika wa klabu hiyo Alexander Isak na ameweka wazi kuwa anaweza akarejea katika kikosi tena.
Kocha huyo alikiri kuwa hawezi kusubiri hadi Jumatatu saa 6:59 usiku dirisha la usajili litakapofungwa, hivyo uamuzi unaweza ukatoka mapema leo.
Isak, ambaye anataka kuondoka na kutua Liverpool iliyo tayari kutoa Pauni 130 milioni kwa ajili ya kumsajili, hajacheza mechi yoyote ya Ligi Kuu England tangu kuanza kwa msimu huu.
Klabu hiyo tayari imemsajili shambuliaji wa kimataifa wa Ujerumani, Nick Woltemade, kwa dau la Pauni 69 milioni ili kuongeza makali katika safu ya ushambuliaji, ambayo ina pengo la Isak ambaye amegoma kabisa kurejea kikosini.
Baada ya sare dhidi ya Leeds katika mechi iliyopigwa kwenye uwanja wa Elland Road, Howe alisema hana "taarifa mpya" kuhusu Isak na hajawasiliana naye kabisa, lakini alisisitiza Newcastle bado inatafuta wachezaji wapya ili kuboresha eneo lao la ushambuliaji.
Akizungumzia hatima ya Isak, alisema:"Kwa kweli sijui. Mimi si sehemu ya mazungumzo yoyote yanayoendelea. Nilikuwa najiandaa kwa mchezo huu ambao ulikuwa mgumu vya kutosha. Mimi pia Nitapata taarifa kama watu wengine watakavyopata."
Hata hivyo, alikataa kufunga mlango wa kumrejesha Isak katika kikosi na akaongeza kuwa bado anaamini mshambuliaji huyo anaweza kurejeshwa kwenye kikosi licha ya kuchukiwa na mashabiki wa Newcastle.
"Ndiyo, kutoka upande wangu nimekuwa nikisema hilo tangu mwanzo. Ikiwa bado yupo chini ya mkataba nasi, sina budi kumrudisha ikiwa itatokea nafasi hiyo"
Baada ya kumsajili Woltemade, Newcastle sasa inapambana kumsajili mshambuliaji wa Brentford, Yoane Wissa, au straika wa Wolves, Jorgen Strand Larsen, kabla ya kuidhinisha kuondoka kwa Isak.
Howe aliongeza:"Kama meneja, kila mara una matumaini ya kupata walau mchezaji mmoja au wawili wanaoweza kuleta tofauti. Lakini nimeridhika sana na kazi tuliyofanya hadi sasa na naamini timu hii ni imara zaidi kuliko msimu uliopita. Tukibahatika, tunaweza kuongeza zaidi wachezaji."