Hizi hapa sababu za Palmer kuuzwa Chelsea

Muktasari:

  • Staa huyo mwenye umri wa miaka 21 aliamua kuachana na maisha ya Etihad kwenda kukipiga Stamford Bridge, ambako amekuwa kwenye kiwango bora sana kwenye Ligi Kuu England msimu huu wa 2023-24.

MANCHESTER, ENGLAND. PEP Guardiola amefichua sababu za Manchester City kuchukua uamuzi wa kumpiga bei Cole Palmer kwenda Chelsea mwaka 2023.

Staa huyo mwenye umri wa miaka 21 aliamua kuachana na maisha ya Etihad kwenda kukipiga Stamford Bridge, ambako amekuwa kwenye kiwango bora sana kwenye Ligi Kuu England msimu huu wa 2023-24.

Palmer alifunga bao kwenye Ngao ya Jamii dhidi ya Arsenal kabla ya kufunga la kusawazisha wakati Man City ilipoichapa Sevilla kwa mikwaju ya penalti kwenye mchezo wa UEFA Super Cup, Agosti 2023. 

Hiyo ndiyo ilikuwa mechi yake ya mwisho Palmer kuichezea Man City kabla ya kutimkia zake kutinga uzi wa The Blues.

Kwa kuwa Riyad Mahrez alikuwa anaondoka Man City kwenda huko Saudi Arabia, hiyo ilidhaniwa kwamba ingeacha nafasi ya kucheza kwa Palmer, lakini ghafla, Guardiola alifanya usajili wa kumleta Jeremy Doku kikosini.

Kuona hivyo, Chelsea ilibisha hodi Etihad na kwenda kumnasa Palmer kwa ada ya uhamisho ya Pauni 42.5 milioni.

Na tangu wakati huo Palmer amekuwa matata kwelikweli mbele ya goli, akifunga mara 20 kwenye Ligi Kuu England na kuchuana na straika wa Man City, Erling Haaland kwenye mbio za kufukuzia Kiatu cha Dhahabu msimu huu.

Guardiola aliulizwa kwanini alimuuza Palmer, alijibu: "Kwenye pre-season nilimwambia abaki kwa sababu Riyad (Mahrez) anaondoka, alisema 'hapaa, nataka kuondoka'."

Guardiola aliongeza: "Alikuwa akitaka kuondoka kwa karibu misimu miwili. Nilimwambia 'hapana, baki'. Tungefanya nini tena?"

Hata hivyo, Guardiola anafichua kwamba hakutumia nguvu nyingi kumshawishi kiungo huyo mshambuliaji kubaki na kama angeongeza juhudu kidogo basi Palmer angekuwapo Etihad kwa sasa. Man City itakipiga na Chelsea kwenye nusu fainali ya Kombe la FA uwanjani Wembley usiku wa leo Jumamosi.


...