Hizi hapa ratiba tatu ngumu NBA hadi ubingwa
Muktasari:
- Kipindi hicho huanza Aprili hadi Juni, ambapo fainali mara nyingi huwa ni katikati hadi mwishoni mwa Juni, lakini kiuhalisia bingwa wa NBA hupatikana Juni.
KWA kawaida Ligi ya Kikapu Marekani ina ratiba tatu ngumu. Kwanza kuna kipindi cha timu zote kucheza katika kanda zao yaani Mashariki na Maghariki na hiki huwa ni kati ya Oktoba hadi Aprili maarufu kama regular season ambako hukipiga kusaka zile zinazotinga mchujo (play off).
Kipindi hicho huanza Aprili hadi Juni, ambapo fainali mara nyingi huwa ni katikati hadi mwishoni mwa Juni, lakini kiuhalisia bingwa wa NBA hupatikana Juni.
Ratiba inaonyesha kwamba inapofika fainali ambayo hulazimu wakati mwingine kucheza mechi saba, kwa msimu huu iko hivi; mchezo wa kwanza utapigwa Juni 3, ilhali ule wa pili ukipigwa Juni 5 na wa tatu Juni 8.
Wa nne utachezwa Juni 10 huku wa tano (ikiwa ni lazima) ukipigwa Juni 13. Mchezo wa sita (ikiwa lazima) Juni 16, 2026 na wa saba (ikiwa ni lazima) utachezwa Juni 19.
Hivyo, kama mechi zitachezwa hadi mchezo wa saba NBA inaweza kumalizika Juni 19. Lakini, je unajua inakuwaje kwa bingwa na MVP? Zipo bonasi tofauti za ubingwa na mchujo.
NBA ina bonasi kwa timu zinazocheza mchujo na kushinda ubingwa, na inagawanywa kwa wachezaji kulingana na jinsi timu zinavyofanikiwa. Mathalani, kwa timu inayoibuka bingwa wa NBA inapata takriban Dola 8.8 milioni.
Hata hivyo, kwa kila mchezaji bonasi huwekwa pamoja na malipo ya ligi na hatimaye huenda kwa wachezaji kulingana na mkataba wa timu. Hii inaweza kumfanya mchezaji apate bonasi kati ya Dola 200,000 hadi zaidi ya Dola 1,000,000 kulingana na mkataba wake binafsi.
NBA pia ina mashindano ya kati ya msimu (NBA Cup) ambayo pia hutoa bonasi ambapo kila mchezaji anaweza kupata Dola 530,000 kama bonasi timu yake ikishinda. Hii ni tofauti na ubingwa wa ligi.