Giannis katikati ya vigogo NBA
Muktasari:
Dirisha hilo linatarajiwa kufungwa Februari 5, ambapo mwaka. Mwaka jana, dirisha la usajili la NBA lilipokuwa linakaribia kufungwa mchezaji mmoja nyota alitoa kauli baada ya dili kubwa lililomhamisha Luka Doncic kwenda Los Angeles Lakers na Anthony Davis kwenda Dallas Mavericks.
OKLAHOMA, MAREKANI: TIMU nyingi zinaweza kuwa zinaandaa ofa kuwania saini ya nyota wa Milwaukee Bucks, Giannis Antetokounmpo wakati tarehe ya mwisho ya usajili wa dirisha dogo la Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) ikikaribia
Dirisha hilo linatarajiwa kufungwa Februari 5, ambapo mwaka. Mwaka jana, dirisha la usajili la NBA lilipokuwa linakaribia kufungwa mchezaji mmoja nyota alitoa kauli baada ya dili kubwa lililomhamisha Luka Doncic kwenda Los Angeles Lakers na Anthony Davis kwenda Dallas Mavericks, alisema:
“Hii ni biashara. Lazima uelewe hilo. Hakuna aliye salama. Hakuna aliye salama.”
Mchezaji aliyesema maneno hayo alikuwa ni Giannis Antetokounmpo ambaye dirisha la usajili la msimu huu linakaribia kufungwa likiwa limebaki chini ya siku tatu, na safari hii ni yeye aliyeko katikati ya mjadala wa biashara.
Tetesi kuhusu mustakabali wake je, Bucks watambadilisha au la? Zitaendelea hadi ama ahamishwe au dirisha lifungwe Alhamisi mchana. Na kama hatahamishwa sasa kuna uwezekano mkubwa tetesi hizo zitarudi tena Juni wakati wa drafti na mwanzo wa usajili wa wachezaji huru.
Hadi juzi Ijumaa kulikuwa na dili moja tu kubwa msimu huu ambapo Atlanta ilimhamisha Trae Young kwenda Washington Wizards.
Kwa wastani kumekuwapo na dili 13 kila dirisha la usajili kwa muongo mmoja uliopita, lakini kwa sasa inaonekana wazi kuwa timu zinasubiri Antetokounmpo ataangukia wapi.
“Nadhani kuna mazungumzo mengi yanaendelea ligi nzima,” alisema meneja mkuu wa Golden State, Mike Dunleavy Jr. wiki iliyopita. “Tunazungumza na timu zote, kila mtu anazungumza na mwenzake, kupima hali.”
“Sina jibu,” alisema kocha wa Bucks, Doc Rivers, Alhamisi alipoulizwa kuhusu tetesi za mchezaji huyo na kuongeza:
“Sijawahi kuwa na jibu. Kila msimu ni tofauti. Sasa ni ngumu zaidi. Nimesema mara nyingi. Zamani ilibidi ununue gazeti ili usome habari.”
Je, Rivers anahangaika na wazo la kumpoteza Antetokounmpo? “Kwa nini ufikirie kitu ambacho hakijatokea na pengine hakitatokea?” alihoji meneja huyo.
Jambo moja liko wazi; timu zote 30 za NBA zimepokea na kupiga simu katika siku chache zilizopita na zitaendelea kufanya hivyo kwa siku chache zijazo zikitaka kujua soko likoje na jinsi zinavyoweza kuboresha vikosi.
Golden State Warriors ni miongoni mwa timu zinazomtaka zaidi Antetokounmpo. Miami Heat pia ni moja ya hizo. New York vivyo hivyo. Kimsingi kila mtu Milwaukee ikiwemo ingependa kuwa naye kwenye kikosi, ingawa ukweli ni kwamba timu nyingi hazina nafasi kubwa ya kufanikisha dili hilo.
“Hatutoi muda mwingi kwa hilo,” alisema kocha wa Miami Heat, Erik Spoelstra, akizungumza kwa ujumla kuhusu tetesi za usajili. “Wachezaji wenye uzoefu wanaelewa kuwa mengi ni nadharia. Ni porojo. Lakini, ni sehemu ya biashara yetu. Hicho ndicho tunachokubali tunaposaini mikataba.”
Kwamba timu zina nia kubwa ya kuwa na Antetokounmpo siyo jambo la kushangaza; bado ni mmoja wa wachezaji bora duniani. Swali kubwa ni kama Milwaukee wanaona huu ndio wakati wa kuachia nguzo yao hiyo ya muda mrefu katikati ya msimu usioridhisha, huku akitarajiwa kuwa nje kwa wiki kadhaa zijazo kutokana na jeraha.
Wiki iliyopita, nyota huyo alionekana akipiga kengele baada ya Milwaukee kupoteza dhidi ya Oklahoma City akisema:
“Hatuchezi kwa bidii. Hatufanyi mambo sahihi. Hatuchezi ili kushinda. Hatuchezi kama timu. Muunganiko wetu haupo. Wachezaji wanafutia mambo yao binafsi. Watu wanajaribu kufanya kila kitu peke yao.”
Msimu unaonekana kuwakimbia Milwaukee na baadhi ya machaguo yao ya baadaye kwenye drafti pia yamekwisha kutokana na mikataba mingine waliyoifanya katika miaka ya hivi karibuni. Walimpata Damian Lillard kisha wakashuhudia akirarua Achilles na hatimaye wakamruhusu aondoke ili arejee Portland. Rekodi yao ni 18-28 wakiwa nafasi ya 12 katika Ukanda wa Mashariki.
Antetokounmpo ambaye alitumia sehemu ya siku ya Alhamisi kwenye hafla ya kumuaga Peter Feigin anayejiuzulu urais wa Milwaukee baada ya miaka 12 yupo miezi michache tu kabla ya kuingia mwaka wa mwisho wa mkataba wake.