Edwards, staa wa tatu mdogo NBA kufikisha pointi 10,000
Muktasari:
Fadeaway ni aina ya mpira wa kurusha (shot) ambapo mchezaji huruka na kurusha mpira huku akirudi nyuma lengo likiwa ni kumpa kazi ngumu mlinzi ili asizuie au kugusa mpira kirahisi. Mara nyingi mpira wa aina hiyo hutupwa mchezaji akiwa bado hewani huku mwili ukirudi nyuma.
MINNEAPOLIS, MAREKANI: ANTHONY Edwards amekuwa mchezaji wa tatu mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) kufikisha pointi 10,000 katika michuano hiyo baada ya nyota huyo wa Minnesota Timberwolves kufunga mpira wa ‘fadeaway’ umbali wa futi 13 kutoka mstari wa pembeni katikati ya robo ya nne dhidi ya Cleveland.
Fadeaway ni aina ya mpira wa kurusha (shot) ambapo mchezaji huruka na kurusha mpira huku akirudi nyuma lengo likiwa ni kumpa kazi ngumu mlinzi ili asizuie au kugusa mpira kirahisi. Mara nyingi mpira wa aina hiyo hutupwa mchezaji akiwa bado hewani huku mwili ukirudi nyuma.
Katika kufikia rekodi hiyo, Edwards maarufu Ant akiwa na umri wa miaka 24 na siku 156, ametanguliwa tu na LeBron James (miaka 23, siku 59) na Kevin Durant (miaka 24, siku 33). Edwards ni mmoja wa wachezaji saba waliowahi kufikisha pointi 10,000 kabla ya kufikisha umri wa miaka 25, akijiunga na kundi linalowajumuisha Kobe Bryant, Luka Doncic, Tracy McGrady na Carmelo Anthony.
“Kusema ukweli ni jambo zuri, lakini najua bado nina safari ndefu mbele yangu, kwa hiyo siyo jambo kubwa sana,” alisema Edwards baada ya ushindi wa pointi 131-122 dhidi ya Cavaliers na kuongeza:
“Kwa kweli inaniumiza kidogo kuwa nimempita Kobe. Nilitamani ningesubiri kama siku 100 hivi, lakini sawa tu.”
Mchezaji huyo alifunga pointi 25, akatoa pasi za mwisho tisa na kunyakua mipira saba ya rebounds, huku Timberwolves wakirekodi viwango vya juu zaidi msimu huu katika asilimia ya kufunga kwa mchezo wa wazi (open play) ikiwa ni 51 kati ya 89 sawa na asilimia 57, na mipira ya pointi tatu (20 kati ya 38, asilimia 53).
Katika mchezo huo Edwards alifunga mipira 10 kati ya 20 ya aina hiyo na minne kati ya saba ya pointi tatu.
“Kufunga pointi huja kwa urahisi kwa njia nyingi,” alisema kocha Chris Finch, akizungumzia mchezo wa kwanza wa pointi 40 kwa Edwards katika kikapu uliochezwa Phoenix mwishoni mwa msimu wake wa kwanza. na kuongeza:
“Wakati huo ulijua kuna kitu ndani yake kinachomruhusu kufikia kiwango hicho.”
Edwards ambaye alikuwa chaguo la kwanza drafti ya 2020, alianza kucheza NBA akiwa na umri wa miaka 19 na amefanikiwa kuzifikia pointi 10,000 katika michezo 412, ikiwa ni kasi ya 28 kwenye historia ya NBA na ya saba kwa kasi miongoni mwa wachezaji wanaoendelea kucheza.
Kwa uchache wa michezo nyota huyo anawafuatia kina Doncic (mechi 358), James (368), Joel Embiid (373), Durant (381), Trae Young (390) na Donovan Mitchell (410).
Ni wachezaji wawili tu wengine waliowahi kufunga pointi 10,000 wakiwa na Timberwolves ambao ni Kevin Garnett na Karl-Anthony Towns.
USAJILI WAENDELEA
Wakati katika soka dirisha dogo la usajili likiendelea kwenye nchi mbalimbali NBA pia mastaa wameanza kupishana katika usajili unaotarajiwa kufungwa Februari 5, mwaka huu.
Hata hivyo, kwa utaratibu wa ligi hiyo mchezaji hawezi kuhamia timu nyingine mpaka dili lake liidhinishwe ndipo anapotangazwa na timu na jana Washington Wizards ilimtangaza mkali maea nne wa All-Star, Trae Young ambaye mchakato wa kuhama ulikamika Januari 9 akitokea Atlanta Hawks alikokuwa akikipiga tangu 2018.
Katika dili hilo la kubadilishana, Hawks imewapokea Christian James McCollum maarufu CJ McCollum aliyedumu kwa msimu mmoja tu Wizards pamoja Corey Kispert (2021-2026).