Henry ampasha Arteta hatutaki kisingizio
Muktasari:
- Arsenal mara ya mwisho kunyakua taji hilo mshambuliaji wao alikuwa Henry na aliweka rekodi kwenye kikosi cha timu hiyo kilichocheza kwa msimu mzima bila ya kupoteza mechi yoyote kwenye Ligi Kuu England, 2003-04.
LONDON, ENGLAND: THIERRY Henry amemwambia Kocha Mikel Arteta majeruhi hayawezi kuwa kisingizio cha kufanya vizuri kwani kinachotakiwa msimu huu Arsenal ni lazima ishinde ubingwa wa Ligi Kuu England.
Arsenal mara ya mwisho kunyakua taji hilo mshambuliaji wao alikuwa Henry na aliweka rekodi kwenye kikosi cha timu hiyo kilichocheza kwa msimu mzima bila ya kupoteza mechi yoyote kwenye Ligi Kuu England, 2003-04.
Arteta na Arsenal yake kwa sasa anaongoza msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi mbili dhidi ya Manchester City wakati huu ikifika katika kipindi hiki cha sikukuu. Lakini, miamba hiyo ya Emirates imekumbwa na majeruhi wengi kikosini, akiwamo beki Ben White, aliyeongeza idadi ya wachezaji majeruhi kwenye kikosi.
Gwiji wa Arsenal, Henry, 48, amesema: “Majeruhi, mechi nyingi, tusizungumze hilo, kila mtu ana matatizo yake. Ngoja tuone hali itakavyokuwa mwisho. Sitaki kubadili msimamo wangu wa tangu mwanzo wa msimu, yatupasa kushinda ubingwa wa ligi. Inapaswa kuwa mwaka huu. Naamini timu inaweza kufanya hivyo natumaini tutaweza kuvuka kizingiti.
“Timu lazima ikumbane na majaribu, majeruhi ni wengi na mambo mengi yanaweza yasiwe unavyotaka. Je, unavukaje?.”
White, 28, alitolewa uwanjani kutokana na kusumbuliwa na maumivu katika mechi ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Wolves.
Maumivu hayo yanaweza kumfanya awe nje ya uwanja kwa muda usiopungua mwezi mmoja.
Na jambo hilo linamfanya beki huyo wa kulia kwenda kuungana na mastaa Gabriel, Kai Havertz na Cristhian Mosquera, wakati William Saliba, Martin Odegaard, Bukayo Saka, Noni Madueke na Gabriel Jesus nao walikosa mechi kadhaa kutokana na kuwa majeruhi.
Arsenal itasafiri kwenda Merseyside kukipiga na Everton katika mchakamchaka wa Ligi Kuu England, kisha Jumanne itacheza na Crystal Palace kwenye robo fainali ya Kombe la Ligi na itafuatia na mechi dhidi ya Brighton, Aston Villa, Bournemouth na Liverpool kwenye kivumbi cha mechi za ligi.