Arteta ataja janga jingine huko
Muktasari:
- Mreno huyo aliyetolewa uwanjani wakati mechi hiyo ikiendelea Jumatano iliyopita, ameiweka Arsenal katika hali mbaya kwani kabla ya kuumia kwake William Saliba na Gabriel Magalhaes walishakuwa nje kutokana na majeraha.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta amethibitisha kuwa Arsenal imepata pigo jingine la majeraha baada ya staa wao aliyesajiliwa katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi, Cristhian Mosquera, aliyeumia katika mechi dhidi ya Brentford kuthibitika kuwa atakaa nje kwa wiki nyingi.
Mreno huyo aliyetolewa uwanjani wakati mechi hiyo ikiendelea Jumatano iliyopita, ameiweka Arsenal katika hali mbaya kwani kabla ya kuumia kwake William Saliba na Gabriel Magalhaes walishakuwa nje kutokana na majeraha.
“Kwa bahati mbaya atakuwa nje kwa muda mrefu kidogo, zaidi ya vile tulivyotarajia bado anahisi maumivu, kwa hivyo atakuwa nje kwa wiki kadhaa,” alisema Arteta baada ya kumalizika kwa mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Club Brugge huko Ubelgiji.
Arsenal ambayo inawania kushinda taji la Ligi Kuu England msimu huu, ushindi huo ulikuwa unairejesha katika mstari baada ya kupoteza dhidi ya Aston Villa Jumamosi iliyopita.
Kichapo hicho kutoka kwa Villa kilikuwa kinahitimisha mfululizo wao wa kucheza mechi 18 za mashindano yote bila ya kupoteza.
Arteta amekuwa akilalamikia sana ratiba ya ligi akieleza kuwa ndio chanzo cha wachezaji wake wengi kukumbwa na majeraha kwa sababu hawapati muda mwingi wa kumpumzika.
“Inafikia muda tunakosa hata wakati wa kufanya mazoezi ya kurudisha miili katika utimamu. Unapokosa baadhi ya wachezaji, unalazimisha wengine kufanya zaidi, mwisho wanajikuta wakipata majeraha. Tuna ratiba ngumu sana, kuna wachezaji wengine wamecheza zaidi ya mechi 150 katika misimu miwili,” alisema.