Hebu msikie Ronaldo anachosema kuhusu Ten Hag, Rangnick

Muktasari:
- Unataka kumfahamu ni makocha gani hao waliopigwa kijembe? Nani, Sir Alex Ferguson au Carlo Ancelotti? Jose Mourinho au Zinedine Zidane?
RIYADH, SAUDI ARABIA: SUPASTAA, Cristiano Ronaldo amefunguka mengi ikiwamo kuwapiga vijembe baadhi ya makocha waliowahi kumnoa hawajui mpira.
Unataka kumfahamu ni makocha gani hao waliopigwa kijembe? Nani, Sir Alex Ferguson au Carlo Ancelotti? Jose Mourinho au Zinedine Zidane?
Mshindi huyo mara tano wa Ballon d’Or amepita kwenye mikono ya makocha wengi katika maisha yake ya soka na hivi karibuni amefunguka kuhusu mabosi wake hao wa zamani, ambao wengine aliwahi kutibuana nao kwa sababu mbalimbali.
Staa huyo wa zamani wa Manchester United amecheza soka chini ya makocha 19 tofauti, ikiwa makocha wa muda. Kwenye orodha hiyo ya makocha, wapo wale mahiri kama Jose Mourinho, Carlo Ancelotti, Sir Alex Ferguson, Zinedine Zidane na Massimiliano Allegri
Chini ya makocha hao watano, Ronaldo alishinda mataji kibao kwenye ligi za England, Hispania na Italia.
Hata hivyo, Ronaldo amewahi kucheza pia chini ya makocha Erik ten Hag, Rudi Garcia na Maurizio Sarri.
Kwenye orodha hiyo, Ronaldo, 39, ametibuana na Ten Hag katika awamu yake ya pili aliyokuwa Man United. Staa huyo wa Ureno aligoma kutolewa kwenye mechi dhidi ya Tottenham Hotspur, Oktoba 2022, jambo lililomfanya awekwe kando kwenye timu. Na Ronaldo aliondoka kabisa Man United baada ya kufanya mahojiano na Piers Morgan na alimsema vibaya kocha huyo jambo lililomfanya mkataba wake kusitishwa. Kwenye mahojiano hayo ya Morgan, ambaye ni shabiki kindakindaki wa Arsenal, CR7 aliwashambulia kwa maneno makali kocha Ten Hag na yule aliyemtangulia uwanjani Old Trafford, Ralf Rangnick.
Sasa amefunguka kuhusu makocha wake wa zamani, akidai wengine walikuwa ovyo kabisa.
Ronaldo aliambia El Chiringuito:
“Nilijifunza kutoka kwa kila mmoja. Nilikuwa na makocha wengine wa ovyo kweli.
“Wengine hawakuwa hata na ufahamu wa soka kabisa.”
Kwenye mahojiano hayo, Ronaldo aliulizwa pia kuhusu upinzani wake wa uwanjani na supastaa wa Kiargentina, Lionel Messi.
Kati ya 2008 na 2023, wawili hao kwa pamoja wameshinda Ballon d’Or mara 13 na Messi ameshinda tatu zaidi ya tano za Ronaldo.
Walimenyana jino kwa jino kwenye La Liga, wakati Ronaldo alipokuwa Real Madrid na Messi kwenye kikosi cha Barcelona.
Hata hivyo, Ronaldo alisema tena kwa msisitizo hakukuwa na uadui wowote baina yao wawili na walikuwa wakielewana sana.
Alisema: “Nina uhusiano mzuri sana na Leo Messi. Nilikuwa namtafsiria Kiingereza kwenye sherehe za tuzo pia. Ilikuwa safi sana, upinzani wenye afya, tunaelewana sana.”
Supastaa Ronaldo, ambaye aliwahi kuzichezea pia Sporting CP na Juventus, alichukua muda wake pia kumshauri Kylian Mbappe na fowadi huyo Mfaransa ametua Real Madrid, hadi sasa ameshafunga mabao 21 katika mechi 33. Ronaldo alisema: “Nampenda sana na si kwa sababu ya stori yake alipokuwa mtoto shujaa wake alikuwa Cristiano Ronaldo, la kwa sababu namwona ni staa anayekuja kwa kasi na kuwapa furaha Real Madrid. Nimekuwa nikimtazama akiwa anacheza kwa sababu mwanangu Mateo anampenda sana Mbappe.
“Nafasi ya ushambuliaji ina mambo magumu na kwa sababu yeye si mshambuliaji halisi kwa maoni yangu. Si kwamba hajui, lakini ile si nafasi yake.
“Ningekuwa pale Real Madrid, ningemfundisha jinsi ya kucheza Namba 9, kwa sababu yeye si mshambuliaji wa eneo hilo. Natumika kama mshambuliaji, lakini nilicheza pia wingi na watu walisahau hilo. Kama ningekuwa yeye, ningecheza kama au zaidi ya Cristiano alivyokuwa akicheza kama mshambuliaji.”
Ronaldo atatimiza umri wa miaka 40 leo, Jumatano na tayari ameshafunga mabao 923 katika maisha yake ya soka.
Kwa Ronaldo yupo Saudi Arabia akikipiga kwenye kikosi cha Al-Nass na msimu huu ameshatikiza nyavu mara 23 katika mechi 25 za michuano yote.