He! Messi, Neymar wamepigwa chini

PARIS, UFARANSA. SUPASTAA, Lionel Messi amepigwa chini kwenye Kikosi Bora cha Msimu kwenye Ligue 1 huku jambo hilo likichochea kauli ya baba yake kudai kwamba mwanaye atarejea Barcelona siku moja. Messi amefunga mabao sita tu kwenye ligi za ndani Ufaransa katika mechi 26 alizocheza, ikiwamo mawili aliyofunga dhidi ya Montpellier wiki iliyopita huku maisha yake ya Parc des Princes yakiwa si matamu sana tangu alipohamia hapo akitokea Barcelona kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana.

PSG ilibeba taji la Ligue 1 mwezi uliopita, lakini mashabiki wa timu hiyo hawataki mastaa wa timu hiyo washangilie na taji.

Wakati Messi akikosa nafasi kwenye kikosi cha msimu cha Ligue 1, wachezaji wenzake wanne wanaocheza timu moja, huku swahiba wake na pacha kwenye safu ya ushambuliaji, Neymar naye jina lake likipigwa chini.

Kylian Mbappe amepata nafasi kwenye timu, huku mastaa wengine watatu wa kutoka PSG ni Marquinhos, Nuno Mendes na kipa Gianluigi Donnarumma, licha ya kucheza mechi 17 tu kati ya 37 zilizocheza kwenye ligi.

Wakali wengine kwenye kikosi ni William Saliba wa Marseille ñ akiungana na staa mwingine wa timu hiyo, Dimitri Payet huku Monaco nayo ikitoa wachezaji wawili, kiungo Aurelien Tchouameni na straika Wissam Ben Yedder huku orodha ya kikosi hicho ikikamilishwa na wakali wawili wa Lens, Jonathan Clauss na Seko Fofana na straika wa Rennes, Martin Terrier.