HE! Martial apinga kauli ya Rangnick

HE! Martial apinga kauli ya Rangnick

MANCHSTER, ENGLAND. KIMEUMANA. Mambo si shwari ndani ya viunga vya Manchester United, hasa kwa kile kinachoendelea hivi sasa pamoja na mastaa wake ambao wameonekana hawana furaha chini ya kocha wa mpito Ralf Rangnick.

Habari ya kushtua ni kumhusu straika wa timu hiyo, Anthony Martial ambaye ameripotiwa kuwa aligoma kucheza mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Aston Villa juzi, kwa mujibu wa Rangnick.

Rangnick alithibitisha kauli hiyo Man United ikitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Aston Villa, huku ikitafsiriwa kuwa huenda Martial analazimisha kuondoka kutokana na kukosa muda mwingi wa kucheza pamoja na kukosa namba ya kudumu kikosini.

Lakini Martial ameibuka na kuandika ujumbe kwenye ukurasa wa Instagram akipinga kauli hiyo ya kocha wake kwamba amegoma kusafiri kwa ajili mchezo huo.

Ujumbe wa Martial umebeba maswali mengi hasa baada ya kauli ya Rangnick kuthibitisha aligoma kujumuishwa kikosini.

Ujumbe wa Martial ameuandika hivi: “Kamwe siwezi kugoma kuichezea Man United, nimecheza hapa kwa muda mrefu wa miaka saba, siwezi kuivunjia heshima klabu pamoja na mashabiki wa Man United.”

Ikumbukwe Martial aliweka wazi anataka kuondoka kutokana na ufinyu wa nafasi kikosi cha kwanza tangu mwaka jana, huku timu kama Sevilla ukionyesha nia ya kumsajili kwa mkopo huku kukiwa na kipingele cha kununuliwa jumla msimu ujao.

Hata hivyo, Rangnick alisema kwa sasa hakuna ofa yoyote iliyowekwa mezani hivyo amemtaka straika huyo wa kimataifa wa Ufaransa kuachana na masuala ya kuondoka katika dirisha hili dogo la usajili linaloendela kwa sasa.

Man United imeweka wazi kama Martial mwenye umri wa miaka 25 ataondoka, basi itakuwa kwa mkopo na hawana mpango wa kumuuza kwa sasa.

Nyota mkongwe wa timu hiyo, Cristiano Ronaldo hivi karibuni alitema cheche akiwaomba wachezaji wenzake kuongeza juhudi kwenye mechi zao kutokana na kiwango cha Man United kuporomoka vibaya huku ikiwa na hatihati ya kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uajo.

Kwa sasa Man United bado imeganda katika nafasi ya saba ikiwa na pointi 32 kwenye msimamo wa EPL, baada ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Aston Villa.

Man United ilianza vyema kwenye mchezo huo ikiwa mbele kwa mabao mawili yaliowekwa kimiani na Bruno Fernandes kabla ya Aston Villa kutibua hali ya hewa na kusawazisha mabao yote kupitia kwa Jacob Ramsey na Philippe Coutinho aliyesajiliwa hivi karibuni kwa mkopo akitokea Barcelona.