He! Juventus haimtaki Pogba

TURIN, ITALIA.KLABU ya Juventus inafikiria kuvunja mkataba wa kiungo, Paul Pogba wenye thamani ya Pauni 130,000 kwa wiki baada ya kufungiwa kutokana na kufeli vipimo vya kuongeza nguvu.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 30 kwa sasa amepigwa 'stop' kwa muda usiojulikana na huenda akatumikia adhabu hiyo kwa muda wa miaka minne kama atakutwa na hatia.
Ripoti ya vipimo vyake vilitolewa baada ya mechi ya Serie A dhidi ya Udinese tangu Agosti 20 hata hivyo, kiungo huyo hakucheza mchezo huo.

Baada ya kusimamishwa na Shirika la kuzuia dawa za kuongeza nguvu Italia, Pogba ana siku chache za kutuma vipimo vingine 'Sample B'.

Sheria ya adhabu matumizi ya dawa za kuongeza nguvu kwa kesi kama hiyo ya Pogba ni miaka minne ikipungua miaka miwili kama ikigundulika alitumia bila kukusudia.

Sasa kutokana hilo, Juventus inafikiria kuvunja mkataba wake na staa huyo wa kimataifa wa Ufaransa kwa mara ya pili na hatakuwa mchezaji wa klabu hiyo msimu huu.

Pogba alisaini mkataba wa miaka minne aliporejea akitokea Manchester United mwaka jana, hiyo inamaanisha amebakiza mkataba wa miaka mitatu kukipiga Juventus.

Lakini kutokana na adhabu iliyotolewa na shirika la kuzuia matumizi ya dawa za kuongeza nguvu kwa wachezaji Juventus italazimika kufanya uamuzi mgumu kuhusu kiungo huyo.

Aliporejea Turin, taarifa ziliripoti Pogba alikubali kukatwa mshahara kutoka Pauni 290,000 hadi Pauni 130,000 kwa wiki.
Aidha wakala wa Pogba, Rafaela Pimenta, alimtetea mchezaji huyo akisema: "Tunasubiri mpaka ishu yake itakapojadiliwa hatutazungumza kitu."