He! Barca yagoma kumuuza kinda wao

BARCELONA, HISPANIA. HABARI ndo hiyo. Barcelona imeripotiwa kugomea ofa ya Pauni 172 milioni kutoka kwa vigogo wa Ulaya waliokuwa wakitaka huduma ya moja ya mastaa wao Nou Camp.

Kinda aliyeibukia kwenye akademia ya La Masia, Lamine Yamal, ndiye aliyetengewa mkwanja mrefu hivyo na miamba ya soka ya Ufaransa, Paris Saint-Germain iliyokuwa ikihitaji huduma yake akakipige Parc des Princes.

Yamal, 16, ameibuka kwa kasi na kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Barcelona, akifunga mabao manne na kuasisti sita kati ya 28 alizocheza kwenye La Liga msimu huu.

PSG ilivutiwa na huduma yake na kuamua kuweka mezani Pauni 172 milioni kwa ajili ya kupata saini ya kinda huyo na rais wa Barca, Joan Laporta alisema: “Tulipokea ofa ya kumhusu mhezaji Lamine Yamal, Euro 200 milioni (Pauni 172milioni), na tumekataa.

“Kwa sababu tunamwaamini kijana wetu, moja ya hazina kubwa kwenye timu. Tupo kwenye mwendo wa kujiweka sawa kiuchumi, hivyo tupo tayari kusubiri hadi mwisho.”.

Kinachoelezwa ni kwamba ofa hiyo iliwasilishwa Nou Camp mapema mwezi huu.

Barcelona ilitangaza kukubaliana mkataba wa miaka minane na Yamal mwaka jana na kwamba makubaliano mapya yatafikiwa wakati atakapofikisha umri wa miaka 18.

Winga huyo si kwamba tu ameibuka kwa kasi kwenye kikosi cha Barca, bali pia amekuwa akipata nafasi kwenye timu ya taifa ya Hispania.

Laporta alisema klabu hiyo haina mpango wowote wa kuuuza vijana wake, akiwamo Pedri, (Alejandro) Balde, Gavi, (Ronald) Araujo, ambao wote ofa zimekuwa zikiletwa.