Haya Arteta apigwa kombora

Muktasari:
- Mfaransa huyo, ambaye ni beki wa kati wa zamani, aliyekuwa nahodha wa Arsenal wakati anacheza, anaamini klabu yake hiyo imeshindwa kupambana kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England na lawama zote ni kwa kocha Arteta.
LONDON, ENGLAND: NAHODHA wa zamani wa Arsenal, William Gallas amemtolea uvivu kocha wa sasa wa miamba hiyo ya Emirates, Mikel Arteta kwamba Mhispaniola huyo si kocha wa viwango vya juu.
Mfaransa huyo, ambaye ni beki wa kati wa zamani, aliyekuwa nahodha wa Arsenal wakati anacheza, anaamini klabu yake hiyo imeshindwa kupambana kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England na lawama zote ni kwa kocha Arteta.
Gallas alisema: "Haikubaliki Arsenal kuendelea kufanya makosa yaleyale ya miaka mitano ndani ya kocha huyo huyo mmoja. Sitaki kusikia visingizio, sitaki kusikia kuhusu majeruhi. Huwezi kuwa na visingizio kama ukiwa na akili ya ushindi. Sidhani kama ana hiyo akili ya ushindi kwa sababu Arsenal ilipaswa walau kuwa na taji moja sasa, au mataji mawili, lakini wala hawapo kwenye mbio.
"Arteta ndiye aliyesababisha, alifahamu wazi kwamba majeruhi yatakuja tu kwenye timu, alifahamu mapema atapoteza wachezaji wake muhimu na ndio maana unahitaji kikosi kikubwa. Kama unataka kushinda, huwezi kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England na wachezaji 11 tu."
Arsenal, ambayo inawafukuzia mastraika Alexander Isak na Benjamin Sesko kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi, ilishindwa kunasa straika wa kiwango cha dunia kwa miaka mitano iliyopita licha ya kulifanya jambo hilo kuwa kipaumbele chao kwenye kila madirisha la usajili.
Gallas akiwa mwenye hasira, alisema uamuzi huo haukubaliki na kudai ishu ya kunasa wachezaji wa viwango vya dunia kwenye usajili ni kitu kinachotazamwa kwa upofu na kocha Arteta.
"Kusajili straika inaonekana ni upofu wa Arteta. Na ndiyo maana Arsenal imemaliza nafasi ya pili kwa misimu miwili mfululizo na huu unakwenda kuwa msimu wa tatu," alisema.