Hawa wachezaji bei zao usiguse!
Muktasari:
- Soka limeshuhudia idadi kubwa ya vijana wanaochipukia kwa kasi kwenye mchezo huo, huku wengi wao wakiwa hata hawajafikisha umri wa miaka 20.
LONDON, ENGLAND: HABARI ndo hiyo. Kuna makinda 10 wa Ligi Kuu England katika orodha ya wanasoka wenye umri mdogo na wenye thamani kubwa kwenye soko la dunia kwa sasa.
Soka limeshuhudia idadi kubwa ya vijana wanaochipukia kwa kasi kwenye mchezo huo, huku wengi wao wakiwa hata hawajafikisha umri wa miaka 20.
Mtandao wa CIES Football Observatory umeweka bayana orodha ya makinda 20 ambao thamani zao zipo juu zaidi sokoni kwenye historia ya mchezo huo kwa sasa.
Na kisichoshangaza ni kwamba, supastaa wa Barcelona, Lamine Yamal ndiye kinda mwenye thamani kubwa zaidi sokoni kwa sasa.
Yamal, 18, thamani yake huko sokoni kwa sasa inatajwa kuwa Pauni 308 milioni hasa baada ya kuonyesha kiwango bora kabisa akifunga mabao 18 na asisti 25 katika mechi 55.
Kinda wa Chelsea, Estevao Willian, 18, anamfuatia staa huyo wa kimataifa wa Hispania kwa mbali, akitajwa kuwa na thamani ya Pauni 104 milioni.
Kinda mwingine wa Barcelona, Pau Cubarsi, 18, anashika namba tatu, akiripotiwa kuwa na thamani inayokadiliwa ni Pauni 99.3 milioni.
Tano bora inakamilishwa na mkali wa Real Madrid, Franco Mastantuono, 18, mwenye thamani ya Pauni 90.2 milioni na kiungo wa Paris Saint-Germain, Warren Zaire-Emery, 19, aliyetajwa kuwa na thamani ya Pauni 81.3 milioni huko sokoni kwa sasa.
Makinda wa Arsenal, Ethan Nwaneri, 18, anayetajwa kuwa na thamani ya Pauni 77.6 milioni na Myles Lewis-Skelly, 19, aliyeripotiwa kuwa na thamani ya Pauni 74.7 milioni wameorodheshwa kwenye 10 bora. Nyota hao wawili wa Arsenal wanaungana na mkali wa Sporting Lisbon, Geovany Quenda mwenye thamani ya Pauni 70.6 milioni, ambaye atatua Chelsea msimu ujao.
Quenda, 18, anafuatiwa na staa wa Real Madrid, Endrick, 19, mwenye thamani ya Pauni 64.5 milioni na mkali wa Tottenham Hotspur, Lucas Bergvall, 19, mwenye thamani ya Pauni 59.9 milioni.
Kinda wa Chelsea, Jorrel Hato, 19, (Pauni 59.1 milioni) na wa Eintracht Frankfurt, Can Uzun, 19, (Pauni 56.8 milioni), pamoja na nyota wa FC Porto, Rodrigo Mora, 18, (Pauni 55.2 milioni) na staa wa Spurs, Archie Gray, 19, (Pauni 47.5 milioni) na kinda wa PSG, Senny Mayulu, 19, aliyetajwa kuwa na thamani ya Pauni 45.4 milioni wameorodheshwa kwenye 15 bora.
Orodha hiyo inakamilishwa na kinda wa Manchester United, Leny Yoro, 19, mwenye thamani ya Pauni 44.4 milioni, staa wa Bournemouth, Eli Junior Kroupi, 19, (Pauni 43.3 milioni), kinda wa FC Porto, Victor Vroholdt, 19, (Pauni 43 milioni), nyota wa Newcastle United, Lewis Miley, 19, (Pauni 39.8 milioni) na yule wa Chelsea, Marc Guiu, 19, aliyeripotiwa kuwa na thamani ya Pauni 38.5 milioni huko sokoni kwa sasa. Hiyo ndiyo orodha ya makinda ghali duniani kwa sasa.