Hawa hapa mastaa 60 huru EPL
Muktasari:
- Kwa mujibu wa ripoti, zaidi ya wachezaji 60 wanatarajiwa kumaliza mikataba yao ifikapo majira ya kiangazi, jambo linaloweza kufungua ukurasa mpya wa usajili na kuibua ushindani wa kuwania saini za nyota hao. Idadi hii kubwa inaashiria wazi kuwa dirisha lijalo la usajili linaweza kuwa miongoni mwa yenye shughuli nyingi zaidi katika historia ya hivi karibuni ya ligi hiyo.
LONDON, ENGLAND: KATIKA kipindi hiki cha mwisho wa msimu wa Ligi Kuu England ambapo Manchester City na Arsenal zibakabana koo kwenye mbio za ubingwa, klabu nyingi kwenye ligi hiyo pendwa duniani zinajiandaa kwa mabadiliko makubwa huku mikataba ya baadhi ya wachezaji ikielekea ukingoni.
Kwa mujibu wa ripoti, zaidi ya wachezaji 60 wanatarajiwa kumaliza mikataba yao ifikapo majira ya kiangazi, jambo linaloweza kufungua ukurasa mpya wa usajili na kuibua ushindani wa kuwania saini za nyota hao. Idadi hii kubwa inaashiria wazi kuwa dirisha lijalo la usajili linaweza kuwa miongoni mwa yenye shughuli nyingi zaidi katika historia ya hivi karibuni ya ligi hiyo.
Miongoni mwa majina yanayoongoza gumzo ni nahodha wa Manchester City, Bernardo Silva, ambaye tayari ametangaza kuondoka baada ya miaka ya mafanikio makubwa. Kuondoka kwake kunatarajiwa kuacha pengo kubwa si tu katika eneo la ubunifu wa safu ya kiungo, bali pia katika uongozi ndani ya kikosi hicho.
Katika Manchester United, hali si tofauti sana. Kiungo mkongwe Casemiro, ambaye amekuwa nguzo muhimu katika kikosi hicho, anatajwa kuwa mbioni kuondoka licha ya kurejea katika kiwango kizuri mwishoni mwa msimu. Uamuzi huu unaweza kuwa sehemu ya mkakati mpana wa klabu hiyo kufanya maboresho ya kikosi chenye mchanganyiko wa vijana na uzoefu.
Upande wa Liverpool, hali inaonekana kuwa ya tahadhari zaidi. Beki wa kushoto Andy Robertson anaripotiwa kuwa katika rada za Tottenham Hotspur huku klabu hiyo ya London ikionekana kuvutiwa na uzoefu wake. Wakati huo huo, hatma ya beki Ibrahima Konate bado haijapatiwa ufumbuzi, jambo linalozua maswali kuhusu mipango ya muda mrefu ya safu ya ulinzi ya Liverpool.
Kwa Arsenal, hali ni tulivu kwa kiasi kikubwa. Klabu hiyo inaonekana kufanikiwa kuwalinda nyota wake muhimu kimkataba huku kipa Karl Hein akiwa ndiye anayetajwa zaidi kuondoka. Utulivu huu unatoa ishara ya mipango madhubuti ya ujenzi wa kikosi chenye mwendelezo.
Aston Villa wao wanaonekana kuwa katika nafasi nzuri zaidi, wakiwa na idadi kubwa ya wachezaji waliofungwa na mikataba ya muda mrefu hadi mwaka 2027.
Hata hivyo, hali ni tofauti kwa Bournemouth, ambapo beki Marcos Senesi anaripotiwa kukataa ofa kadhaa za kuongeza mkataba. Endapo ataondoka, klabu hiyo italazimika kutafuta mbadala mwenye uwezo wa kuziba pengo hilo muhimu katika safu ya ulinzi.
Kwa upande wa Brighton & Hove Albion, changamoto kubwa ni uwezekano wa kuwapoteza wachezaji wenye uzoefu kama James Milner na Adam Webster.
Burnley wanakabiliwa na hali ngumu zaidi, hasa iwapo watashuka daraja. Katika mazingira kama hayo ni kawaida kwa wachezaji wengi kuondoka ili kusaka changamoto mpya, hali itakayohitaji ujenzi upya wa kikosi.
Kwa Chelsea, sera ya kutoa mikataba mirefu kwa wachezaji inaendelea kuwa kinga dhidi ya kupoteza nyota wao kwa urahisi.
Crystal Palace wanaweza kuwaaga viungo wao Jefferson Lerma na Daichi Kamada, ambao mikataba yao inaelekea mwisho.
Everton wanatafakari kuongeza mkataba wa kiungo mkongwe Idrissa Gueye ambaye bado ana mchango mkubwa licha ya umri wake.
Kwa Fulham, Harry Wilson ameibuka kuwa miongoni mwa wachezaji wanaowindwa zaidi kufuatia msimu mzuri aliouonyesha.
Leeds United nao wanakabiliwa na maamuzi muhimu, huku kipa Karl Darlow akiwa miongoni mwa wachezaji wanaokaribia kumaliza mikataba yao. Newcastle United tayari wamepata pigo la kumpoteza beki wao muhimu Kieran Trippier ambaye amethibitisha kuondoka. Hii inalazimu klabu hiyo kuingia sokoni kusaka mbadala atakayeweza kudumisha kiwango cha ushindani.
Kama ilivyo kwa klabu nyingine Nottingham Forest, Sunderland na West Ham United nazo zitakuwa na mabadiliko kwenye vikosi vyao.