Harry Kane mezani kwake dili ni kubaki Bayern
Muktasari:
- Nahodha huyo wa timu ya taifa ya England, 32, angeweza kuondoka kwa ada ya Pauni 56.7 milioni dirisha lijalo la majira ya kiagazi endapo angewajulisha Bayern Munich kabla ya mwisho wa Januari anataka kuondoka.
MUNICH, UJERUMANI: STRAIKA, Harry Kane yuko kwenye mazungumzo ya kuongeza mkataba wake Bayern Munich, jambo linalozima matumaini ya klabu zilizokuwa zikivizia kipengele chake cha kuachiliwa kwa bei nafuu.
Nahodha huyo wa timu ya taifa ya England, 32, angeweza kuondoka kwa ada ya Pauni 56.7 milioni dirisha lijalo la majira ya kiagazi endapo angewajulisha Bayern Munich kabla ya mwisho wa Januari anataka kuondoka.
Hata hivyo, dalili zote sasa zinaonyesha Kane ataendelea kubaki Allianz Arena, ambako amekuwa akifunga mabao mengi na hatimaye kufungua ukurasa wa kutwaa mataji katika maisha yake ya soka.
Nahodha huyo wa zamani wa Tottenham ana mkataba na Bayern hadi majira ya joto ya 2027, lakini bosi wa klabu hiyo, Max Eberl, amesema mipango ya kurefusha mkataba wake tayari imeanza.
Alipoulizwa kuhusu mazungumzo ya mkataba mpya, Eberl aliiambia Sky Germany: “Tuko kwenye mazungumzo na Harry.”
Awali, Kane alitarajiwa kurejea England ili kujaribu kuvunja rekodi ya Alan Shearer ya mabao 260 kwenye Ligi Kuu England.
Kocha wa Spurs, Thomas Frank amesema mwezi Septemba Kane angekuwa “karibu zaidi ya kukaribishwa” kurejea Kaskazini mwa London.
Lakini Kane, ambaye bado yuko nyuma ya mabao 47 kufikia rekodi ya Shearer, ameonekana kupoa kuhusu wazo la kurejea England angalau kwa sasa.
Amesema mwaka jana: “Nina furaha sana hapa Munich. Familia yangu imeshaanza kuzoea maisha hapa. Watoto wangu wanafurahia shule zao. Haya ndio maisha yangu hapa kwa kipindi kijacho. Nadhani bado tuna mwanzo tu wa kipindi kizuri sana cha mafanikio kwa klabu hii na nataka kuwa sehemu ya hilo.”
Klabu za Ligi Kuu zingesimama foleni kumsajili mshambuliaji huyo, ambaye alifunga mabao 280 katika mechi 435 alizochezea Spurs.
Hata hivyo, takwimu zake Ujerumani zimekuwa za kushangaza zaidi, akiwa amefunga mabao 119 katika mechi 126 kwa jumla, na mabao 34 katika mechi 30 msimu huu.