Dili jipya la Kane lipo tayari mezani
Muktasari:
- Mkataba wa nahodha huyo wa England, Kane, 32 unatarajia kumalizika wakati wa majira ya kiangazi 2027 na ndani yake kuna kipengele cha kuvunjwa endapo kama kutakuwa na timu itakayokuwa tayari kulipa ada ya uhamisho iliyotajwa katika dirisha hili la usajili wa Januari.
MUNICH, UJERUMANI: STRAIKA, Harry Kane amefichua kuwa mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya Bayern Munich yanatarajiwa kufanyika muda wowote kuanzia sasa.
Mkataba wa nahodha huyo wa England, Kane, 32 unatarajia kumalizika wakati wa majira ya kiangazi 2027 na ndani yake kuna kipengele cha kuvunjwa endapo kama kutakuwa na timu itakayokuwa tayari kulipa ada ya uhamisho iliyotajwa katika dirisha hili la usajili wa Januari.
Hata hivyo, licha ya kuonekana kuwa hakuna klabu itakayojaribu kuamsha kipengele hicho katika dirisha la usajili la Januari, hilo haliwezi kuzuia uvumi kuhusu mustakabali wake.
Klabu za Ligi Kuu England zimehusishwa na mpango wa kumsajili Kane wakati wa dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Tottenham Hotspur inaweza kujaribu kumrudisha mshambuliaji wao wa kihistoria, huku kocha Thomas Frank akifungua mlango mapema msimu huu kwa Kane kurejea. Lakini, kauli za Kane katika miezi ya hivi karibuni zimepunguza uwezekano huo.
Kane anaweza kuvunja rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote katika Ligi Kuu England, akizingatiwa kuwa kwa sasa yupo nafasi ya pili nyuma ya Alan Shearer.
Ingawa Kane amekiri kuwa mazungumzo yatafanyika, amesema anataka kuzingatia kuendelea kwa msimu baada ya mapumziko ya majira ya baridi.
Amesema: “Ndiyo, inawezekana kabisa. Asilimia 100. Haya ni mazungumzo ambayo yanapaswa kufanyika, kama nilivyosema kabla ya mapumziko ya baridi. Nina uhakika yatafanyika, lakini kwa sasa mtazamo wangu uko kwenye msimu huu. Kuna fursa kubwa. Hakuna mahali ningependa kuwa zaidi ya hapa kwa sasa.”
Hata hivyo, rais wa heshima wa Bayern Munich, Uli Hoeness, alifichua mwaka 2025 kuwa kipengele hicho huisha kila mwezi Januari. Ada inayohitajika kuamsha kipengele hicho ni Pauni 57 milioni, kitu ambacho kinawezekana kwa timu zenye uwezo tu wa kiuchumi kutumia kiasi kama hicho kwa sasa kwenye dirisha la katikati ya msimu.
Tangu alipotua Bayern akitokea Spurs kwa ada ya Pauni 100 milioni, Kane amefunga mabao 115 katika mechi 121 kwa klabu hiyo. Msimu huu ameshafunga mabao 30 katika michuano yote.