Harry Kane kawa mtamu kinyama yani!
Muktasari:
- Nahodha huyo wa kikosi cha Three Lions, anayeichezea Bayern Munich kwa sasa mwaka jana kampuni yake inayosimamia haki za taswira zake ilikuwa na thamani ya Pauni 11 milioni, wakati akiwa na mali nyingine zinazokabiliwa kuwa na thamani ya Pauni 15 milioni.
MUNICH, UJERUMANI: STRAIKA, Harry Kane ameripotiwa kuwa na pato linalofikia thamani ya Pauni 100 milioni kwa sasa huku hilo likinganishwa na thamani yake ya mabao anayofunga kila siku, yanayotajwa kuwa na thamani ya Pauni 200,000.
Nahodha huyo wa kikosi cha Three Lions, anayeichezea Bayern Munich kwa sasa mwaka jana kampuni yake inayosimamia haki za taswira zake ilikuwa na thamani ya Pauni 11 milioni, wakati akiwa na mali nyingine zinazokabiliwa kuwa na thamani ya Pauni 15 milioni.
Staa huyo wa zamani wa Tottenham mwenye umri wa miaka 32, anavuna pia pesa kutoka kwa kampuni za Nike, Mars na watengeneza viatu Skechers.
Aliwekwa kwenye orodha ya matajiri ya Sunday Times Rich List ya Mei mwaka jana, alipotajwa kuwa na pato linalofikiwa Pauni 100 milioni na tangu wakati huo pesa zimeongeza. Kampuni yake ya haki za taswira inayoitwa HK28 Limited iliingiza Pauni 11,428,513.
Na uwekezaji wake umekuwa kutoka Pauni 2.8 milioni hadi Pauni 5.1 milioni kuanzia 2023. Wadhamini wake pia wamemwingizia Pauni 723,000, huku akilipa kodi ya Pauni 566,000 kutoka kipato chake alizopata kabla ya makato ya kodi Pauni 2.3 milioni.
Kwa thamani hiyo ya Kane, hiyo ina maana mabao yake 489 aliyofunga katika maisha ya soka kuanzia Leyton Orient, Leicester, Tottenham, Bayern na England kuwa na thamani zaidi ya Pauni 204,000 kwa kila bao.
Straika huyo anaripotiwa kulipwa Pauni 400,000 kwa wiki kutokana na huduma yake anayotoa huko Bayern na ndio kwanza anaelekea kwenye nusu ya mkataba wake wa miaka minne, ambao utamfanya akusanye Pauni 86 milioni kupitia mshahara.