Harry Kane hii sasa sifa, afanya kufuru
Muktasari:
- Kane alikamilisha hat-trick yake kwa kuunganisha krosi ya Olise, na kufanya Bayern kuweka rekodi ya Bundesliga ya kufunga mabao zaidi ya moja katika mechi 21 mfululizo.
MUNICH, UJERUMANI: Harry Kane alitoka benchi na kufunga hat-trick wakati Bayern Munich walipokuwa na ushindi mkubwa wa 5-0 dhidi ya VfB Stuttgart ushindi wao wa 72 ambao ni rekodi katika Bundesliga na kuongeza uongozi wao hadi pointi 11 kileleni.
Kocha Vincent Kompany aliwapa mapumziko baadhi ya wachezaji wake muhimu akiwemo Manuel Neuer na Kane.
Hata hivyo Bayern hawakuchelewa kutikisa nyavu, wakifungua ukurasa kupitia Konrad Laimer aliyehitimisha mpira murua wa ushirikiano na Michael Olise.
Stuttgart waliokuwa hawajawahi kukosa bao msimu huu, walijaribu kurudi mchezoni, lakini juhudi zao zinakataliwa kwa ofsaidi na kupiga nje.
Kane alipoingia, hakuhitaji muda dakika tano tu baada ya kuingia alifunga bao zuri kwa shuti la chini kutoka yadi 25.
Kipa Alexander Nubel alifanya makosa yaliyowapa Bayern bao la tatu, na baadaye alisababisha penalti baada ya kuzuia mpira kwa mkono, ambayo Kane aliifunga kwa ustadi.
Kane alikamilisha hat-trick yake kwa kuunganisha krosi ya Olise, na kufanya Bayern kuweka rekodi ya Bundesliga ya kufunga mabao zaidi ya moja katika mechi 21 mfululizo.