Bosi Bayern afichua kipengele cha Kane
Muktasari:
- Straika huyo wa kimataifa wa England mkataba wake kwenye kikosi cha Bayern Munich utafika tamati 2027, huku ripoti zikidai kwamba kuwapo na kipengele kinachotaja bei anayoweza kuuzwa kinaripotiwa kitakwenda kuzua vita kali kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
MUNICH, UJERUMANI: RAIS wa heshima wa Bayern Munich, Uli Hoeness amefichua kwamba kipengele kinachotaja bei anayouzwa straika Harry Kane kitafika ukomo wake mwishoni mwa Januari 2026.
Straika huyo wa kimataifa wa England mkataba wake kwenye kikosi cha Bayern Munich utafika tamati 2027, huku ripoti zikidai kwamba kuwapo na kipengele kinachotaja bei anayoweza kuuzwa kinaripotiwa kitakwenda kuzua vita kali kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Gazeti la Ujerumani la Bild liliripoti kwamba kwenye mkataba wa sasa wa Kane kuna kipengele kinachotaja Pauni 57 milioni kuwa ndiyo kiasi kinachofaa kuvunja mkataba wake na kitaanza kufanya kazi kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Ripoti zinafichua kwamba straika huyo anaweza kuondoka Bayern kwa bei hiyo ndogo kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi na kubainisha pia uwezekano wa kuondoka kabla ya kufungwa kwa dirisha la uhamisho la Januari.
Kane amekuwa na kiwango bora katika kikosi hicho cha mabingwa wa Bundesliga msimu huu, akifunga mabao 24 katika mechi 20. Jambo hilo ndilo linalomfanya Kane aanze kuhusishwa na klabu nyingine kubwa za Ulaya ikiwamo Barcelona.
Lakini, bosi wa heshima wa Bayern, Hoeness alisema kipengele hicho kinachosema Kane anaweza kuondoka kwa pesa ndogo kitafika tamati kwenye dirisha la Januari pekee.
Hoeness aliambia Bild: "Yeye (Harry Kane) ana hicho kipengele kila mwaka na kinafika tamati mwishoni mwa Januari. Tuna uhakika anaheshimu mkataba wake hadi 2027. Hata ingekuwa sisi, tungemfuata pia, tunaamini ataongeza mkataba. Familia yake ina furaha sana. Hapa Munich, unaweza kuendelea na biashara zako kwa amani. Harry Kane alikuwa akitembea anaongozana na walinzi kule kwao (London). Sidhani kama anahitaji maisha ya aina hiyo hapa."
Uli Hoeness amekuwa akijihusisha na Bayern Munich tangu 1970, alipojiunga akiwa mchezaji.
Kuhusu Kane, ameshafunga mabao 109 katika mechi 116 alizochezea Bayern kwa misimu miwili na aliiwezesha timu hiyo kubeba ubingwa wa Bundesliga msimu uliopita.