Harry Kane ataja wabaya wa England
Muktasari:
- Sasa, England'Three Lions' wanaelekeza nguvu zao kwenye Kombe la Dunia 2026, na nahodha wao Harry Kane ametaja timu ambazo anaamini zitakuwa tishio kubwa kwao katika harakati za kutwaa ubingwa.
MIAMI, MAREKANI: ENGLAND haijashinda Kombe la Dunia la FIFA katika kipindi cha miaka 60 iliyopita. Mara yao ya kwanza na mwisho kutwaa taji hilo ilikuwa mwaka 1966 walipokuwa wenyeji wa mashindano hayo.
Sasa, England'Three Lions' wanaelekeza nguvu zao kwenye Kombe la Dunia 2026, na nahodha wao Harry Kane ametaja timu ambazo anaamini zitakuwa tishio kubwa kwao katika harakati za kutwaa ubingwa.
Akizungumza kabla ya mashindano hayo, mshambuliaji huyo wa Bayern Munich aliulizwa kuhusu timu zenye nguvu zaidi kwenye mashindano hayo.
"Nadhani zipo kadhaa. Kama ilivyo katika kila mashindano makubwa, kuna Ufaransa, Argentina, Brazil na Hispania. Kuna timu nyingi nzuri sana. Unaweza kupitia orodha ndefu ya timu, na hiyo ndiyo inayofanya mashindano haya kuwa magumu," alisema.
Kane aliendelea kusema:"Siyo rahisi kama timu mbili tu kucheza dhidi ya kila mmoja. Kuna mambo mengi yanayohusika, na tunahitaji kuwa tayari kwa yote hayo. Lakini ndiyo, hizo ni baadhi ya timu ambazo bila shaka zitakuwa tishio."
Chini ya kocha Thomas Tuchel, England inaingia Kombe la Dunia ikiwa na matumaini makubwa ya kumaliza ukame wa mataji ya kimataifa na kushinda ubingwa wa dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1966.
Kane mwenyewe anaingia mashindanoni akiwa katika kiwango bora baada ya kufunga mabao 61 katika mechi 51 kwa Bayern Munich msimu huu na kutwaa Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya. Pia ndiye mfungaji bora wa muda wote wa England akiwa na mabao 79 katika mechi 113.
Aidha, Kane anaweza kuwa mfungaji bora wa England katika historia ya Kombe la Dunia. Kwa sasa ana mabao 8, mawili tu nyuma ya rekodi ya Gary Lineker.
Kabla ya kuanza kampeni yao ya Kombe la Dunia, England katika mechi ya mwisho ya kirafiki dhidi ya Costa Rica ilipata ushindi wa mabao 3-0.
Katika Kundi L la Kombe la Dunia 2026, England itaanza safari yake dhidi ya Croatia tarehe 17 Juni, kisha itacheza na Ghana tarehe 23 Juni na kumalizia hatua ya makundi dhidi ya Panama tarehe 27 Juni.
Iwapo England itaendelea kuonyesha kiwango chake kizuri, inaweza kuandika historia kwa kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya pili.