Messi avunja rekodi, atuma ujumbe Kombe la Dunia
Muktasari:
- Messi aliingia uwanjani akitokea benchi dakika ya 69 na kufunga bao la pili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 72, akiiwezesha Argentina kushinda 2-0.
MIAMI, MAREKANI: MSHAMBULIAJI Lionel Messi alikuwa miongoni mwa wachezaji walioangaza katika ushindi wa Argentina dhidi ya Iceland katika mechi yao ya mwisho ya maandalizi kabla ya Kombe la Dunia.
Messi aliingia uwanjani akitokea benchi dakika ya 69 na kufunga bao la pili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 72, akiiwezesha Argentina kushinda 2-0.
Bao hilo lilikuwa la kihistoria kwani lilimfanya Messi kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kufunga bao kwa Argentina, akivunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na gwiji wa zamani Angel Labruna.
Baada ya mchezo, Messi alieleza furaha yake ya kurejea uwanjani baada ya kusumbuliwa na tatizo la kiafya tangu alipowasili kambini.
"Nimefurahia tangu mwanzo. Nilikuwa natamani kupata dakika za kucheza baada ya changamoto niliyokuwa nayo tangu nilipowasili. Nina furaha, ninafurahia kila wakati na nina hamasa kama kawaida."
"Nilijisikia vizuri sana. Nilikuwa nataka kuanza kucheza na kuondoa hofu inayokuja unapokuwa na maumivu ili uweze kucheza kwa uhuru. Bado tuna wiki moja kuhakikisha kila mtu yuko tayari kwa mechi ya kwanza," alisema Messi.
“Hili ni kundi lenye wachezaji wenye moyo wa ushindi”
Messi pia aliwatumia mashabiki wa Argentina ujumbe wa matumaini, akiahidi kuwa timu hiyo itafanya kila iwezalo kutafuta nyota ya nne ya ubingwa wa dunia.
"Kama kawaida mashindano makubwa yanapoanza, hasa Kombe la Dunia, kuna hamasa kubwa. Nilisema awali kuwa kundi hili halitawaangusha mashabiki, na limethibitisha hilo mwaka huu bila kujali mpinzani au mashindano. Bado linaonyesha njaa ileile ya ushindi na ushindani. Hili ni kundi lenye moyo wa ushindi ambalo daima linataka zaidi."
Aliongeza kuwa Argentina itachukua kila mechi hatua kwa hatua, lakini kwa imani kubwa katika uwezo wao.
"Kundi hili linastahili kila kitu kizuri kinacholitokea. Tutajaribu kama ambavyo tumekuwa tukifanya siku zote. Mashabiki wasiwe na shaka kwamba tutatoa kila kitu tulichonacho. Wapinzani wetu watapata wakati mgumu kutushinda kwa sababu hii ni timu yenye ushindani mkubwa."
Kupitia akaunti yake ya Instagram, Messi pia aliandika ujumbe mfupi wa kuhamasisha wafuasi wa Argentina:
"Twende mbele, tukiwa pamoja zaidi kuliko wakati mwingine wowote," aliandika sambamba na picha za mechi dhidi ya Iceland.