Harry Kane afunguka, autaja ubingwa Bundesliga

Muktasari:
- Kapteni huyo wa timu ya taifa ya England alifunga bao lake la 25 katika mechi ya kukabidhiwa taji dhidi ya Borussia Monchengladbach ambayo mabingwa hao walimaliza kwa ushindi wa mabao 2-0.
MUNICH, UJERUMANI: STRAIKA wa Bayen Munich, Harry Kane ambaye amenyanyua taji lake la kwanza katika soka la kiushindani wikiendi iliyopita baada ya Bayern kukabidhiwa kombe lao la Ligi Kuu England amesema taji hilo lina maana kubwa kwake kuliko hata tuzo mbalimbali alizowahi kushinda.
Kapteni huyo wa timu ya taifa ya England alifunga bao lake la 25 katika mechi ya kukabidhiwa taji dhidi ya Borussia Monchengladbach ambayo mabingwa hao walimaliza kwa ushindi wa mabao 2-0.
Kane alisema kuwa tuzo ya kiatu cha Dhahabu ya Ligi Kuu ya England aliyoshinda mara tatu, na kile cha Kombe la Dunia mwaka 2018, haviwezi kulinganishwa na kuchukua ubingwa wa Bundesliga na kuvalishwa medali ya kwanza ya ubingwa shingoni mwake.
Kane amewahi kufeli mara kadhaa katika fainali za michuano mbalimbali na mbio za ubingwa wa ligi hali iliyosababisha awe anasemwa sana kwamba ana uwezo mkubwa lakini hajawahi kushinda kombe lolote katika maisha yake ya soka la kiushindani.
Baada ya kunyanyua ndoo hiyo ya Bundesliga Kane alisema: “Imekuwa safari ndefu. Hii inamaana kwangu kuliko tuzo yoyote ya ufungaji bora, hakika. Hakuna siri kwamba hiki ndicho kitu kimoja kilichokuwa kinakosekana katika historia yangu ya soka. Ilikuwa kama mzigo mkubwa juu ya mabega yangu, na sasa nimeunyanyua. Nimepata tuzo nyingi na nimewahi kuwa karibu sana na kushinda mataji tena mara nyingi, lakini kwa sababu moja au nyingine, sikuwahi kufanikiwa.”
“Unapopitia msimu mzima, milima na mabonde, kazi, mazoezi, kisha mnapata nafasi ya kusherehekea namna hii mwisho wa msimu, ni jambo zuri sana kwa sababu sijawahi kukutana na hali hii hapo awali.”
Baada ya filimbi ya mwisho na hafla ya kutunukiwa medali na kukabidhiwa taji, Kane ambaye kwa kawaida ni mtu mtulivu, alionekana akimwangiwa sana bia na wachezaji wenzake ikiwa ni sehemu ya utamaduni wa kusheherekea ubingwa wa Bundesliga kwa Bayern.
Huo ulikuwa ni ubingwa wa 33 wa Bundesliga kwa Bayern ambao wamelitwaa taji hilo baada ya kulipoteza kwa Bayern Leverkusen msimu uliopita.