Hamilton arudi uwanjani baada ya msiba wa mbwa wake 'Roscoe'
Muktasari:
- Hamilton, raia wa Uingereza, alionekana kwa mara ya kwanza katika eneo la mashindano ya Formula 1 tangu alipotangaza kuwa Roscoe alifariki akiwa mikononi mwake Jumapili jioni, baada ya kuugua nimonia kwa mara ya pili mwaka huu 2025.
DEREVA wa timu ya Ferrari, Lewis Hamilton alijizuia kulia alipofunguka kuhusu mapenzi makubwa aliyopokea kufuatia kifo cha mbwa wake Roscoe, akiliita tukio hilo kuwa la kushtua kihisia.
Hamilton, raia wa Uingereza, alionekana kwa mara ya kwanza katika eneo la mashindano ya Formula 1 tangu alipotangaza kuwa Roscoe alifariki akiwa mikononi mwake Jumapili jioni, baada ya kuugua nimonia kwa mara ya pili mwaka huu 2025.
Roscoe, ambaye Hamilton alimchukua mwaka 2013, alikuwa maarufu katika matukio ya Formula 1, baada ya kupewa ruhusa ya kudumu kuhudhuria mashindano hayo huku akiwa kipenzi cha mashabiki sambamba na bingwa huyo wa dunia mara saba.
Baada ya taarifa za kusikitisha, mashabiki wengi walionyesha upendo mkubwa kwa Hamilton na mkufunzi wa Roscoe, Kristin McMillan, ambaye Hamilton mwenye umri wa miaka 40 alimshukuru kwa kumpa mbwa huyo maisha marefu na yenye furaha.
Wakati wa mahojiano na vyombo vya habari katika mashindano ya Grand Prix ya Singapore, Hamilton ameelezea jinsi alivyoathirika kutokana na msiba huo na akagusia mapokezi makubwa aliyoyapata kutoka kwa mashabiki wa Formula 1.
Amesema: "Nimepokea ujumbe kutoka kwa mashabiki wengi sana. Kwa kweli ni jambo lililonishtua kuona ni watu wangapi Roscoe aliwagusa duniani kote. Ni jambo lililogusa moyo sana. Sikuweza kujibu kila mtu.
"Alikuwa kitu cha muhimu zaidi maishani mwangu, kwa hiyo ilikuwa ni hali ngumu sana. Najua watu wengi duniani wamepitia hali kama hii kupoteza mnyama aliyekupenda bila masharti, ni uzoefu wa kipekee. Sasa naangalia mbele, nitarudi kwenye mashindano ya magari na kufanya kile ninachopenda hapa."
Hamilton, ambaye bado hajaanza ushindani tangu ajiunge na timu ya Ferrari msimu huu, ameongeza kuwa anajisikia mwenye matumaini kuelekea mbio hizo baada ya kuzoea gari vizuri zaidi.
Mwenza wake, Charles Leclerc, ameeleza kuwa gari la Ferrari huwa linafanya vizuri zaidi katika hali ya hewa ya joto, na alikubaliana na matumaini ya Hamilton kuwa timu ya Scuderia itaonyesha maendeleo.