Hali ya hewa ni shida Kombe la Dunia

Muktasari:
- Wachezaji wa timu hizo zote walitakiwa kuondoka uwanjani dakika ya 55 kutokana na onyo la hali mbaya ya hewa. Miamba hiyo ya Argentina, Boca ilikuwa imefungana 1-1 na timu hiyo ya ridhaa kutoka New Zealand wakati mechi inasimamishwa.
MIAMI, MAREKANI: HALI ya hewa imeendelea kuwa shida kwenye fainali za Kombe la Dunia la Klabu huko Marekani baada ya kipute cha Boca Juniors na Auckland City kulazimisha kusimamishwa kwa muda.
Wachezaji wa timu hizo zote walitakiwa kuondoka uwanjani dakika ya 55 kutokana na onyo la hali mbaya ya hewa. Miamba hiyo ya Argentina, Boca ilikuwa imefungana 1-1 na timu hiyo ya ridhaa kutoka New Zealand wakati mechi inasimamishwa.
Mwamuzi Glenn Nyberg alichukua uamuzi huo wa kusimamisha mechi kutokana na tishio la radi huko Nashville. Timu hizo zilirejea uwanjani dakika 40 baadaye, huku Boca ikipata taarifa kwamba imeshatupwa nje baada ya Benfica kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bayern Munich.
Na hilo liliathiri kiwango chao baada ya mechi kuendelea na Auckland na timu hiyo kufanikiwa kupata matokeo mazuri kabisa yenye historia yao.
Mechi hiyo ilikuwa ni mara ya tano kwenye fainali za Kombe la Dunia la Klabu kusimamishwa kutokana na hali mbaya ya hewa. Mechi ya Ulsan na Mamelodi ilisimama kwa saa moja kutokana na radi. RB Salzburg na Pachuca ilisimama kwa dakika 90 kutokana na sababu hiyohiyo.
Radi pia ilisababisha mechi ya Palmeiras na Al Ahly kusimamishwa kwa dakika 40.
Na Auckland City si wageni wa jambo hilo, ambapo mechi yao ya Benfica nayo ilisimamishwa kwa saa mbili.
Hali ya hewa Amerika imekuwa ya joto kali kiasi cha kufikia nyuzijoto40 kwenye miji na kutangazwa kuwa ni hali ya hatari. Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca alilalamikia hali hiyo na kusema imewapa wakati mgumu na kukaribia kabisa kushindwa kufanya mazoezi.
Hali hiyo ya hewa inaibua wasiwasi mkubwa katika kuelekea fainali zijazo za Kombe la Dunia 2026, ambazo zitafanyika Marekani, Canada na Mexico. Kuna wasiwasi pia kusimamisha mechi kunaweza kuwafanya mashabiki kuondoka viwanjani, huku wachezaji wakiwa kwenye hatari ya kupata mshtuko kutokana na joto, kuchoka na kuishiwa maji au kupata majeraha mengine yanayotokana na joto kuwa kali.
Mechi nyingine ya Kundi G itazishuhudia Wydad Casablanca ikimenyana na Al-Ain katika mechi ya kukamilisha tu hatua ya makundi kwa upande wao kutokana na timu hizo zote mbili tayari zimeshatupwa nje ya mikikimikiki hiyo.