Hakuna jinsi, Arsenal lazima iuze mastaa
Muktasari:
- Mabosi wa Arsenal wamekuwa wakimuunga mkono Kocha Mikel Arteta kwa nguvu zote katika soko la usajili katika misimu ya hivi karibuni baada ya timu hiyo kurejea tena kuwa miongoni mwa zinazowania ubingwa chini ya kocha huyo Mhispaniola.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL huenda ikalazimika kuuza angalau mchezaji mmoja wa kikosi cha kwanza dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi baada ya kutumia fedha nyingi katika misimu ya karibuni wakijaribu kumaliza ukame wa miaka 22 bila ubingwa wa Ligi Kuu England.
Mabosi wa Arsenal wamekuwa wakimuunga mkono Kocha Mikel Arteta kwa nguvu zote katika soko la usajili katika misimu ya hivi karibuni baada ya timu hiyo kurejea tena kuwa miongoni mwa zinazowania ubingwa chini ya kocha huyo Mhispaniola.
Hata hivyo, matumizi makubwa ya fedha katika madirisha ya usajili yaliyopita sasa yanaweza kuwalazimu viongozi wa klabu kufanya maamuzi magumu mwishoni mwa msimu huu, ikiwemo kuuza baadhi ya wachezaji muhimu wa kikosi cha kwanza.
Kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la The Telegraph, Arsenal ilitumia jumla ya Pauni 268 milioni kwenye ada za usajili katika mwaka uliopita wa kifedha. Kutokana na hali hiyo, klabu italazimika kuuza baadhi ya wachezaji ili kusawazisha matumizi.
Nahodha wa Arsenal Martin Odegaard ni mmoja wa wachezaji ambao klabu inaweza kufikiria kumuuza ikiwa wataamua kumtoa mchezaji ambaye anaweza kuleta ofa kubwa ya fedha sokoni. Kiungo huyo wa kimataifa wa Norway atabakiwa na miaka miwili katika mkataba wake mwishoni mwa msimu huu, jambo linalomaanisha bado ana thamani kubwa katika soko la usajili.
Ripoti hiyo inaeleza baada ya kutumia miaka mitano katika klabu hiyo, kumuuza Odegaard kwa ada kubwa ya uhamisho kunaweza kuipa Arsenal faida kubwa chini ya sheria za matumizi ya fedha za Ligi Kuu ya England na UEFA.
Wachezaji wengine wawili wanaotajwa kuwa na uwezekano mkubwa wa kuondoka ni Gabriel Martinelli na Ben White. Martinelli alijiunga na Arsenal mwaka 2019 kwa ada ndogo ya takribani Pauni 7 milioni, hivyo thamani yake katika vitabu vya klabu bado ni ndogo na kuuza kwake kunaweza kuleta faida kubwa. Ben White naye alinunuliwa kutoka Brighton mwaka 2021 kwa ada ya Pauni 50 milioni.
Katika miaka ya hivi karibuni, klabu nyingi zimekuwa zikiuza wachezaji waliotoka katika akademi zao ili kusaidia kusawazisha matumizi ya fedha.
Kwa upande wa Arsenal, vijana Myles Lewis-Skelly na Ethan Nwaneri, ambao kwa sasa hawako katika kikosi cha kwanza cha Arteta, wanaweza pia kuuzwa. Kai Havertz, kama ilivyo kwa Odegaard, atabakiwa na miaka miwili katika mkataba wake na anaweza pia kuuzwa kwa ada kubwa, sambamba na mastaa wengine kama Leandro Trossard na Gabriel Jesus waliobakiza mwaka mmoja katika mikataba yao, nao wanaweza kuuzwa.