Arsenal yanogewa na Piero Hincapié, kumsajili moja kwa moja
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa kutoka gazeti la The Sun, Arsenal imeamua kutumia kipengele cha kumnunua jumla beki huyo kwa dau la pauni milioni 45 (Sh153 bilioni). Utaratibu huu unatarajiwa kufanana na ule wa mlinda mlango David Raya, ambaye alianza kwa mkopo kabla ya kusajiliwa moja kwa moja.
KLABU ya Arsenal imeripotiwa kuridhishwa na kiwango cha beki wa kimataifa wa Ecuador, Piero Hincapié, tangu ajiunge na timu hiyo kwa mkopo akitokea Bayer Leverkusen, na sasa imepanga kumsajili jumla.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka gazeti la The Sun, Arsenal imeamua kutumia kipengele cha kumnunua jumla beki huyo kwa dau la pauni milioni 45 (Sh153 bilioni). Utaratibu huu unatarajiwa kufanana na ule wa mlinda mlango David Raya, ambaye alianza kwa mkopo kabla ya kusajiliwa moja kwa moja.
Wakati Hincapié akitarajia usajili wa moja kwa moja, ripoti kutoka gazeti la Daily Telegraph imezua mshangao baada ya kudai kuwa Arsenal imewaweka sokoni wachezaji wanne muhimu: Gabriel Martinelli, Ben White, pamoja na makinda Ethan Nwaneri na Myles Lewis-Skelly.
Sababu za Arsenal kutaka kuwauza mastaa hao ni pamoja na kanuni za fedha baada ya kutumia zaidi ya pauni milioni 250 msimu uliopita, klabu inahitaji kuuza wachezaji wa kikosi cha kwanza ili kusawazisha hesabu na kufanikisha usajili wa kudumu wa Hincapié.
Jambo lingine ni ushindani wa namba ambapo Gabriel Martinelli amepoteza nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza mbele ya Eberechi Eze na Leandro Trossard.
Pia ujio wa Jurriën Timber ni sababu ya Ben White kujikuta akiwa mchezaji wa ziada kutokana na kuimarika kwa kiwango cha Mholanzi huyo.
Uamuzi wa kuwaweka sokoni makinda kama Nwaneri na Lewis-Skelly unatajwa kama hatua ya hatari, lakini Arsenal inajikuta katika shinikizo la kuingiza fedha ili kuendelea kuimarisha kikosi hicho chini ya kocha Mikel Arteta.