Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kocha KMC afichua siri ya mastaa Brazil

Muktasari:

  • Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, kocha huyo ameeleza namna ambavyo taifa lake lilivyofanikiwa kuanzisha mfumo unaozalisha mastaa wa dunia kila kukicha ambao unaunganisha vipaji vya mitaani kabla ya kuanza kucheza soka la kulipwa katika klabu mbalimbali.

MBRAZILI wa KMC, Wilson Toledo ambaye ni msaidizi wa Marcio Maximo amefichua kile anachokiita siri ya mafanikio ya Brazil katika soka la dunia akisema Tanzania inaweza kufika huko kama itaamua kuwekeza kikamilifu katika misingi ya maendeleo ya wachezaji chipukizi.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, kocha huyo ameeleza namna ambavyo taifa lake lilivyofanikiwa kuanzisha mfumo unaozalisha mastaa wa dunia kila kukicha ambao unaunganisha vipaji vya mitaani kabla ya kuanza kucheza soka la kulipwa katika klabu mbalimbali.

“Brazil haijawa taifa kubwa kwa bahati mbaya. Ni matokeo ya utamaduni wa mpira uliojengeka kwenye maisha ya kila mtoto. Tofauti na mataifa mengine, huko mpira sio burudani tu ni njia ya maisha,”€  anasema Toledo.


MAFANIKIO YA BRAZIL

Akifafanua zaidi Toledo anasema wachezaji wengi wa Brazil huanza safari ya soka wakiwa mitaani wakicheza ‘futsal’ kwenye maeneo madogo yaliyosheheni changamoto. Mchezo huo unaochezwa kwa kasi unawasaidia kukuza uwezo wa kumiliki mpira, kuwa na akili ya haraka na ubunifu sifa ambazo zimeonekana kwa mastaa kama Neymar, Vini­cius Jr na Ronaldinho.

“Watoto wengi nchini Brazil hawaanzi kwenye uwanja mkubwa wa nyasi. Wanaanza kwenye mitaa yenye vumbi, kwenye futsal. Huko wanajifunza kufanya maamuzi haraka, kudhibiti mpira. Ni shule isiyo rasmi, lakini ndiyo msingi wa kila mchezaji mkubwa,”€  anasema Toledo.

Anaongeza kuwa kwa wastani mchezaji wa Kibrazili huanza kushiriki katika akademi za klabu akiwa na umri wa miaka 15 au 16, muda ambao tayari anakuwa na uzoefu wa kutosha wa mitaani.

Tunapomchukua kijana wa miaka 16, tayari anajua kitu kuhusu mpira. Hapo tunabaki kumfundisha nidhamu, mazoezi ya mwili na falsafa ya timu. Ndiyo maana wachezaji kama Estevao Willian, Endrick au Vini­cius wamekuwa nyota mapema walitoka kwenye mfumo unaoweka msingi tangu utotoni,”€  anasema.


VIPAJI VYA TANZANIA

Toledo anasema tangu alipoanza kufanya kazi nchini, amevutiwa na kiwango cha asili cha vipaji vya wachezaji wa Kitanzania. Kwa mtazamo wake, Tanzania ina wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kiufundi, nguvu na akili ya mchezo lakini kinachokosekana ni misingi ya uendelezaji na mazingira bora ya kukuza vipaji.

“Nimekuwa nikifanya kazi na vijana wengi hapa KMC na nimeona kuna kitu cha kikubwa ndani yao. Wana nguvu, wana kasi na wana kiu ya mafanikio. Kama wangepata misingi mizuri wakiwa wadogo, nina uhakika Tanzania ingeweza kuwa kama Brazil ya Afrika,”  anasema.

Anaeleza zaidi kuwa, katika mataifa kama Brazil, kila mkoa una vituo vya kuibua vipaji na kufundisha watoto wadogo misingi ya soka kuanzia upigaji wa pasi, kucheza katika nafasi na namna ya kufanya maamuzi. Huko, kila shule au mtaa ni kama chuo cha mpira.

“Hapa Tanzania, nikiona kijana anayecheza vizuri mtaani, mara nyingi hana pa kwenda. Hakuna mfumo wa kumchukua na kumlea. Hilo ndilo jambo la kubadilisha,”€  anashauri Toledo.


WABRAZILI KUSTAAFU MAPEMA

Toledo pia amezungumzia utamaduni wa wachezaji wa Brazil kustaafu mapema, akisema si kwa sababu ya kuchoka, bali ni matokeo ya maisha marefu ndani ya mpira.

“Kijana anayeanza kucheza akiwa na miaka minane au tisa akifika 32 tayari ana miaka zaidi ya 20 ya mpira wa ushindani. Wengi huamua kuwekeza kwenye ukocha, biashara, au familia. Ni sehemu ya mzunguko wa maisha yetu,”€  anasema.

Anaongeza kuwa mfumo huo hufanya kila mchezaji kuwa na hamasa kubwa ya kufanya vizuri mapema, kwani anajua atakuwa na muda mfupi wa kucheza kiwango cha juu kabla ya kugeukia maisha mengine.


TANZANIA KAMA BRAZIL

Akizungumzia maisha yake nchini, Toledo anasema Tanzania inamkumbusha Brazil kwa mambo mengi kuanzia hali ya hewa, watu wenye upendo, hadi mapenzi ya soka.

“Tanzania ni nyumbani kwangu pia. Joto, mazingira, hata watu wenyewe wanapenda mpira. Nilipofika Dar es Salaam nilihisi niko Rio de Janeiro. Hivyo sina changamoto yoyote kubwa ya kuzoea,”€  anasema huku akitabasamu.

Anaeleza kuwa miongoni mwa changamoto chache ni miundombinu ya mafunzo na upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya mazoezi lakini anaamini mabadiliko hayo yanawezekana endapo viongozi wataweka mkazo kwenye maendeleo ya vijana.


SIMBA NA YANGA

Toledo hakusita kugusia watani wa jadi, Simba na Yanga akisema ndizo nguzo kuu zinazobeba hadhi ya soka la Tanzania na endapo zitawekeza zaidi kwenye akademi zao, zinaweza kuwa mfano barani Afrika.

“Simba na Yanga ni kama Flamengo na Palmeiras kule Brazil. Zina mashabiki wengi, zinaheshimika, na zina uwezo wa kifedha. Kama zikitumia nafasi hiyo kuunda shule bora za mpira, basi Tanzania haitakuwa tena taifa la kutazama Kombe la Dunia kupitia televisheni, bali itakuwa ikishiriki,” anasema.


MWENENDO WA KMC

Kuhusu KMC ambayo imekuwa na mwanzo mgumu wa msimu baada ya kupoteza mechi minne mfululizo, Toledo anaamini bado kuna matumaini makubwa. Anasema tatizo kubwa haliko kwenye ubora wa wachezaji, bali kwenye kujiamini na nidhamu ya kimfumo.

“KMC ni timu nzuri. Wachezaji wana uwezo, lakini wakati mwingine wanakosa imani. Unajua unapopoteza michezo kadhaa mfululizo, akili ya mchezaji hubadilika. Sisi kazi yetu ni kuwarudisha kwenye hali ya ushindi, kuwaonyesha kuwa wanaweza kushinda tena,”€  anasema Toledo.

Kocha huyo anaongeza kuwa yeye na kocha mkuu Maximo wamekuwa wakifanya kazi kubwa kurejesha morali ya timu kwa kuzingatia nidhamu ya mazoezi, mifumo ya kiufundi na kuhimiza umoja wa wachezaji katika kikosi wanachofundisha.