Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Haaland: Man City Vs Arsenal….Sitasahau!

HALAAND Pict

Muktasari:

  • Haaland amezungumzia mvutano huo akisema hakuamini mechi iliisha bila majeraha, akieleza tukio la mgongano wa vichwa lilimfanya ahisi ameumia vibaya, lakini baadaye ikawa hofu tu ya muda.

MANCHESTER, ENGLAND: HAIKUWA rahisi. Kwa mashabiki wa soka duniani jana zilipigwa mechi nyingi katika ligi mbalimbali, lakini lile bato kati ya Manchester City na Arsenal kwenye Ligi Kuu England ndilo lililogeuka gumzo kutokana na vita ya ubingwa ilivyo baina ya timu hizo.

Na baada ya mchezo walikuwa ni Manchester City walioondoka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wageni wao uwanjani Etihad, hivyo kupunguza pengo la pointi kuwa tatu, huku Man City wakiwa na mchezo mmoja mkononi. Katikati ya mchezo huo kulikuwa na misuguano ya wachezaji ndani ya uwanja. Arsenal wanaongoza wakiwa na pointi 70, huku Man City wakiwa nazo 67.

Lakini, bato kali miongoni mwa wachezaji lilikuwa katika eneo la ushambuliaji la Man City lililoongozwa na kinara wa ufungaji mabao, Erling Haaland dhidi ya beki wa Arsenal, Gabriel Magalhaes, ambapo muda wote walikuwa ng’adu kwa ng’adu. Baada ya mchezo, Haaland amesema hatawasahau mabeki wa Arsenal walivyombana katika pambano hilo kali.

Haaland amezungumzia mvutano huo akisema hakuamini mechi iliisha bila majeraha, akieleza tukio la mgongano wa vichwa lilimfanya ahisi ameumia vibaya, lakini baadaye ikawa hofu tu ya muda.

HALA 01

Katika mchezo huo, Haaland na Magalhaes walivutana, kusukumana na kupigania nafasi kila wakati. Mambo yalizidi kuwa makali zaidi Magalhaes alipoonekana kumgonga Haaland kichwani katika tukio lenye utata ndani ya boksi. Licha ya ukali huo, wote walipewa kadi za njano, jambo lililozua mjadala mkubwa kwa watazamaji na wachambuzi wa soka.

Haaland amesema mtindo wake wa uchezaji unalenga matokeo zaidi kuliko ubishi wa uwanjani: “Mechi kama hizi huwa na mipambano mingi. Wakati mwingine ni vita ya nani ashinde pambano la moja kwa moja. Nilifunga bao, kwa hiyo nilishinda wakati huo. Lilikuwa muhimu sana na tulishinda mechi.”

Bao lake la dakika ya 65 ndilo lililoipa Manchester City ushindi huo muhimu, likionyesha tena uwezo wake wa kuamua mechi katika nyakati za presha kubwa.

HALA 02

Pia alizungumzia uamuzi wa mwamuzi kuhusu tukio lake na Gabriel, akisema: “Nadhani kama ningedondoka chini, labda ingekuwa kadi nyekundu. Lakini mimi sianguki kirahisi. Yeye alinijia usoni, lakini ndivyo ilivyo kwenye soka.”

Kauli hiyo imezua mjadala mpana kuhusu tabia ya wachezaji kujiangusha au kubaki imara, ambapo baadhi wanaona kukataa kwake kuanguka kunaonyesha ujasiri, lakini wengine wanaamini inaweza kuwa imeigharimu timu yake kupata faida ya kadi kwa mpinzani.

Hii si mara ya kwanza kwa Haaland na Magalhaes kukutana katika mechi ya aina hiyo ya nguvu, ambapo kila mara mvutano wao umeacha simulizi kubwa baada ya mchezo. Kadri mbio za ubingwa zinavyozidi kupamba moto, matukio kama haya yanaweza kuwa na athari kubwa si tu kwenye pointi, bali pia kwenye akili za wachezaji na mipango ya makocha.

HALA 03

SIKIA HII

Kinachoendelea England sasa ni utani unaoumiza kati ya mashabiki wa timu hizo mbili. Katika eneo moja la jiji, mashabiki wa Manchester City wameweka kibanda cha muda wakiuza kile wanachokiita “machozi ya Arsenal” kwa Pauni mbili kwa chupa, jambo lililogeuka gumzo mitaani na mitandaoni. Wengine wamekuwa wakiimba kwa kejeli “Mikel Arteta, imetokea tena,” wakimaanisha historia ya kupoteza ubingwa inarudia.

Na sasa ikiwa Man City watashinda mechi yao ya kiporo dhidi ya Burnley, wanaweza kupanda kileleni kwa mara ya kwanza tangu Agosti mwaka jana, hali inayoongeza presha kwa Arsenal ambao bado wana ndoto ya kubeba ubingwa walioupoteza tangu msimu wa 2003/2004.

HALA 04

Hata hivyo, makocha Arteta na Pep Guardiola walikubaliana kuwa ushindi wa City wa mabao 2-1 haujamaliza mbio za ubingwa, bali umezifungua zaidi. Guardiola amesema: “Nani anaongoza ligi? Sisi siyo. Hiyo mechi imetupa matumaini tu.”

Kwa muda mwingi wa msimu, Arsenal wameonekana kama timu yenye nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa, lakini wamekumbwa na changamoto ya kumalizia nafasi zao mbele ya lango. City nao wameimarika zaidi baada ya mabadiliko ya kikosi na kuanza kurejea kwenye kiwango cha juu kadri msimu unavyokaribia mwisho.

Hata hivyo mbio bado ziko wazi. Arsenal wana mechi tano zilizosalia dhidi ya timu zilizo chini ya nusu ya jedwali pamoja na nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Atletico Madrid, jambo linaloongeza presha ya ratiba nzito.

Lakini historia inawaumiza zaidi. Msimu wa 2022-23 waliongoza ligi kwa siku 248 lakini wakapitwa na Manchester City mwishoni. Msimu huu wameongoza kwa siku 208 hadi sasa, na bado wana hatari ya kurudia maumivu hayo.Swali kubwa lililosalia ni kama Arsenal wataweza kuvuka presha hii hadi mwisho au wataangukia tena kwenye simulizi ile ile ya “machozi ya Arsenal” ambayo mashabiki wa wapinzani wanaitumia kama silaha ya utani.