Arsenal vs Man City, kuna nini nyuma ya pazia?
Muktasari:
- Manchester City, kikosi cha kocha Pep Guardiola kilitumia vizuri fursa hiyo kwa kuifumua Chelsea nyumbani kwa mabao 3-0, na sasa tofauti kati ya timu hizo mbili ni pointi sita kabla ya mechi baina yao kubwa leo, Jumapili. Kwa msaada wa kompyuta ya utabiri wa Opta, The Athletic inajaribu kujibu swali la nani atamaliza akiwa wa kwanza?
LONDON, ENGLAND: KULIKUWA na mabadiliko ya kushangaza wikiendi iliyopita, ambapo Arsenal ilipoteza nyumbani kwa mabao 2-1 dhidi ya Bournemouth, jambo lililofungua nafasi kwa Manchester City kupunguza pengo katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
Manchester City, kikosi cha kocha Pep Guardiola kilitumia vizuri fursa hiyo kwa kuifumua Chelsea nyumbani kwa mabao 3-0, na sasa tofauti kati ya timu hizo mbili ni pointi sita kabla ya mechi baina yao kubwa leo, Jumapili. Kwa msaada wa kompyuta ya utabiri wa Opta, The Athletic inajaribu kujibu swali la nani atamaliza akiwa wa kwanza?
NINI KIMEBADILIKA GEMU ZILIZOPITA?
Kwa kifupi, ubingwa sasa uko mikononi mwa timu zote mbili, ambapo Arsenal imebaki na pointi 70 baada ya kucheza mechi 32 kufuatia kupoteza dhidi ya Bournemouth, huku Man City ikiwa nazo 64 baada ya mechi 31 kufuatia ushindi dhidi ya Chelsea. Ikiwa Man City itaifunga Arsenal na pia kushinda mechi yake moja iliyo nayo mkononi dhidi ya Crystal Palace, Mei 22, timu hizo zitakuwa na pointi sawa zikitofautishwa na idadi ya mabao.
Hata hivyo, hilo linategemea pia timu hizo zikishinda mechi zilizobaki. Kwa kuwa timu nyingi bado zinapigania malengo, kumaliza msimu bila kupoteza siyo jambo la uhakika. Ukiangalia historia ya karibuni, Man City inaweza kuwa na matumaini zaidi msimu unapoelekea mwisho. Imepoteza mechi moja kati ya 40 za mwisho za Ligi Kuu England katika miezi ya Aprili na Mei, na imeshinda mechi 19 za mwisho za nyumbani mfululizo. Mara ya mwisho kupoteza pointi nyumbani katika kipindi hicho ilikuwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Liverpool Aprili 2022 matokeo ambayo hayakuathiri ubingwa kwani ilishinda kwa tofauti ya pointi moja.
Kwa upande wa Arsenal, haijawa na matokeo ya kuridhisha sana katika miezi hiyo katika misimu ya karibuni ikiwa imetoka sare mara saba na kupoteza mara 11 katika mechi 39 tangu msimu wa 2021-22. Historia siyo lazima itabiri siku zijazo, lakini dalili hizo zinaanza kujitokeza. Hakuna shaka kuwa mechi ya leo ni muhimu katika kuamua mwelekeo wa mbio za ubingwa.
NANI ANAONEKANA KUWA IMARA ZAIDI?
Manchester City imezifunga Arsenal, Liverpool na Chelsea tangu mapumziko ya kimataifa ya Machi, mwaka huu ikifunga mabao tisa bila kuruhusu hata moja. Kama inavyoelezwa kipindi cha mwisho wa msimu huwa ndio wakati wao wa kuonyesha kiwango cha juu zaidi.
Ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Chelsea ulijengwa kwenye mwanzo bora wa kipindi cha pili cha mechi hiyo, ambapo Rayan Cherki alitoa asisti mbili za mabao - krosi nzuri kwa Nico O’Reilly na safi kwa Marc Guehi kusaidia kuvunja mwanya na kuipa Man City ushindi rahisi.
Ujumuishwaji wa Cherki kwenye kikosi cha kwanza umeibua mjadala mkubwa hasa baada ya Guardiola kusema hapo awali kuwa timu ilikuwa ‘haijapangika vizuri’ mwanzoni mwa msimu walipocheza pamoja na Erling Haaland na Jeremy Doku. Hata hivyo, sasa inaonekana kocha huyo ameridhika na mchanganyiko wa ubunifu na uimara wa timu.
Kwa pamoja, safu ya ushambuliaji ina utofauti mkubwa na ni vigumu kuidhibiti kuanzia kasi ya Doku hadi mbinu za Cherki. Hii inaweza kuwa tishio kubwa kwa safu imara ya ulinzi ya Arsenal. Hata hivyo, Arsenal bado ina sababu ya kuwa na matumaini. Licha ya matokeo mabaya ya hivi karibuni wanaongoza ligi na pia wana nafasi ya kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Msimu wao umejikita katika uimara wa safu ya ulinzi. Hawaruhusu mabao mengi wakiwa na wastani wa mabao 0.72 kwa kila dakika 90 ambacho ni kiwango bora barani Ulaya. Hii inawapa msingi imara wa kujenga mashambulizi dhidi ya wapinzani wao.
NANI ANA RATIBA NGUMU ZAIDI?
Kwa sasa, Arsenal bado ina nafasi nzuri zaidi ikiongoza kwa pointi sita na pia ina ratiba nyepesi kidogo kulinganisha na Manchester City.
Arsenal itacheza mechi tatu za nyumbani dhidi ya Newcastle United , Fulham na Burnley. Hata hivyo, inaweza kupata changamoto dhidi ya West Ham United ugenini, timu ambayo imekuwa na kiwango kizuri hivi karibuni.
Katika mechi ya mwisho, watasafiri kwenda Selhurst Park kucheza na Crystal Palace katika uwanja mgumu, ingawa Palace inaweza kuwa na inawazia mashindano ya Ulaya. Kwa upande wa Man City wana mechi ngumu ugenini dhidi ya Bournemouth na Everton, ambazo zinapigania nafasi za kufuzu mashindano ya Ulaya msimu ujao. Pia watacheza dhidi ya Aston Villa ambao wanaweza kuwa tayari wamefikia malengo kufikia wakati huo.
UTABIRI INASEMAJE?
Wiki iliyopita, kompyuta ya utabiri wa matokeo na ubingwa ya Opta ilikuwa imeipa Arsenal nafasi ya asilimia 97.3 kushinda ubingwa. Lakini baada ya kupoteza dhidi ya Bournemouth nafasi hiyo imeshuka hadi asilimia 86.1, huku Manchester City ikiongezewa hadi asilimia 13.9.
Licha ya hayo, Arsenal bado ina nafasi kubwa kutokana na uongozi wa pointi sita, na hata matokeo ya sare, leo, Jumapili, yanaweza kutosha kuizuia Man City katika vita vilivyo mbele ya safari.
Hata hivyo, asilimia ya Man City inaonekana ndogo kuliko uhalisia, hasa ukizingatia mambo kama morali ya timu na hali ya kisaikolojia ambayo haiwezi kupimwa kirahisi kwa takwimu.