Guinea ya Ikweta matatani ikishindwa kuifuata Malawi kufuzu Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Timu hiyo inayonolewa na kocha Juan Micha Obiang, bado iko katika mji mkuu Malabo, Guinea ya Ikweta ambapo wachezaji na benchi la ufundi wanakaa katika hoteli iliyopo eneo la Sipopo.
Guinea ya Ikweta imeshindwa kusafiri kwenda Malawi kwa ajili ya mechi ya kufuzu Kombe la Dunia la FIFA 2026 iliyopangwa kuchezwa jioni ya leo Alhamisi Oktoba 9, 2025, hali iliyozua sintofahamu kuhusu hatma ya mechi hiyo ya Kundi H uliotarajiwa kuchezwa kwenye Iwanja wa Bingu.
Timu hiyo inayonolewa na kocha Juan Micha Obiang, bado iko katika mji mkuu Malabo, Guinea ya Ikweta ambapo wachezaji na benchi la ufundi wanakaa katika hoteli iliyopo eneo la Sipopo.
Kikosi hicho kilikuwa kipange kuondoka Jumatano asubuhi, lakini safari hiyo ilihairishwa ghafla kwa sababu ambazo bado hazijawekwa wazi.
Shirikisho la Soka la Guinea ya Ikweta limeitisha kikao cha dharura leo na linatarajiwa kufanya mashauriano zaidi na maafisa wa serikali ili kutafuta suluhisho la tatizo hilo. FIFA tayari imejulishwa rasmi kuhusu hilo.
Malawi ilikuwa imepanga kuandaa mechi hiyo katika Uwanja wa Taifa wa Bingu uliopo Lilongwe, kama sehemu ya mechi za mzunguko wa pili wa kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026, ambalo litaandaliwa kwa pamoja na Marekani, Canada na Mexico.
Adhabu ya kosa hilo
Guinea ya Ikweta tayari imekumbwa na pigo kubwa katika kampeni ya kufuzu, baada ya FIFA kuwaadhibu Mei kwa kumtumia mchezaji asiye halali, Emilio Nsue, katika mechi za awali.
Kutokana na hilo, timu hiyo ilipokonywa ushindi katika mechi mbili ambazo sasa zimehesabiwa kama vichapo vya 3-0 kwa mujibu wa sheria.
Adhabu hizo zimeathiri nafasi ya Guinea ya Ikweta katika msimamo wa kundi, kwani wamepoteza pointi muhimu na tofauti ya mabao kuharibika.
Nsue, aliyekuwa mfungaji bora katika AFCON 2023, pia alipigwa marufuku ya miezi sita kucheza mechi za kimataifa.
Yatibuliwa kufuzu
Kwa sasa, Tunisia inaongoza Kundi H na ushindani kwa nafasi ya kwanza inayohakikisha kufuzu moja kwa moja umeongezeka. Namibia ipo nafasi ya pili, huku Malawi na Guinea ya Ikweta zikilingana kwa pointi (10) lakini zikitofautiana idadi ya mabao.
Malawi na Guinea ya Ikweta sasa wanakabiliwa na kazi ngumu ya kufuzu, kwani mechi chache tu zimebaki. Malawi, ambao wana faida ndogo ya tofauti ya mabao, wanaweza kunufaika endapo mechi hiyo itahesabiwa kuwa ushindi kwao kwa sababu ya Guinea ya Ikweta kutofika uwanjani. Hata hivyo, bado watahitaji matokeo mazuri katika mechi zao zijazo, pia kutegemea wapinzani wao wakumbwe na matokeo mabaya.
Kwa upande wa Guinea ya Ikweta, nafasi yao ya kufuzu imebaki kuwa finyu sana. Mchanganyiko wa matatizo ya nje ya uwanja na adhabu kutoka FIFA umeweka matumaini yao ya kufuzu katika hali tete.
FIFA na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) bado hawajatoa tamko kuhusu hatma ya mechi hiyo iliyohairishwa au hatua yoyote ya kinidhamu kutokana na kutofika kwa timu hiyo.