Guardiola kuondoka Man City, Matthias Sammer afichua siri
Muktasari:
- Guardiola kwa sasa ana mkataba na Man City hadi 2027, lakini kumekuwa na tetesi zinazoendelea kuwa anaweza kumaliza safari yake ya takribani miaka 10 klabuni mwishoni mwa msimu.
MANCHESTER, ENGLAND: WAKATI Manchester City ikibeba ubingwa wa Kombe la Carabao mwishoni mwa wiki iliyopita, anga la soka la England lilibaki kuwa na swali la ni lini kocha wa kikikosi hicho, Pep Guardiola ataondoka katika kikosi hicho alichokipa mataji zaidi ya 10 katika kipindi cha miaka 10 aliyodumu Etihad.
Na hilo limekuwa likijirudia mara kwa mara katika siku za karibuni kutokana na sintofahamu inayoendelea hasa baada ya kuwapo kwa taarifa katika siku za karibuni kwamba anaweza kuondoka wakati wowote, huku zingine zikidai msimu huu utakuwa wa mwisho kuinoa timu hiyo.
Lakini, katikati ya mjdala huo mkurugenzi wa zamani wa michezo wa Bayern Munich, Matthias Sammer, amezungumzia suala la Guardiola akiamini kwamba kocha huyo anaondoka Manchester City katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi kutokana na kuwepo kwa mambo asiyofurahishwa nayo.
Guardiola kwa sasa ana mkataba na Man City hadi 2027, lakini kumekuwa na tetesi zinazoendelea kuwa anaweza kumaliza safari yake ya takribani miaka 10 klabuni mwishoni mwa msimu.
Ripoti kutoka tovuti ya Daily Mail zilieleza awali kuwa Guardiola anatarajiwa kufanya uamuzi kuhusu mustakabali wake katika kipindi cha mapumziko ya mechi za kimataifa.
Sammer, ambaye aliwahi kufanya kazi na Guardiola kwa miaka mitatu akiwa Bayern Munich, amesema kocha huyo anapaswa kuondoka ili kurejesha nguvu na ari yake.
Akizungumza kupitia Sky Germany, Sammer amesema kuwa licha ya ushindi wa Kombe la Carabao kuonyesha kuwa kila kitu kiko sawa kwa Man City, kuna ishara zinazonyesha mambo yapo tofauti.
“Nilifurahi sana kufanya kazi naye. Tulifanya kazi pamoja vizuri kwa miaka mitatu. Ni mtu ambaye huwa namuelewa vizuri kwa kuangalia tu ujio wake, ishara zake, macho yake na namna anavyozungumza. Hisia zangu zinaniambia kuna kitu hakipo sawa kwa sasa mara zote ninapomuangalia usoni,” amesema.
Sammer pia aligusia hali ya Guardiola kukosolewa hivi karibuni, hasa kuhusu maamuzi ya upangaji wa kikosi katika Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo Man City ilitolewa na Real Madrid katika hatua ya 16 bora. Sammer, mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or mwaka 1996, aliongeza kuwa anapomtazama Guardiola, hakuhitaji maelezo zaidi kwani kila kitu kinajieleza: “Ningemshauri kwa sasa apumzike kidogo na kupata nguvu mpya.”
Kwa sasa, Man City bado inapambana kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England, lakini wako nyuma kwa pointi tisa dhidi ya vinara Arsenal. Hata hivyo, bado ina mchezo mmoja mkononi na itakutana na Arsenal kwenye Uwanja wa Etihad mwezi ujao katika mechi muhimu. Vilevile, itacheza dhidi ya Liverpool katika robo fainali ya Kombe la FA.
Licha ya mashaka kuhusu mustakabali wake, baada ya fainali ya Carabao Cup, Guardiola amesema timu yake itakuwa bora zaidi msimu ujao.
MAFANIKIO YA GUARDIOLA MAN CITY
Ubingwa EPL (6).
Ligi ya Mabingwa (1)
Ubingwa FA (1)
Ubingwa Carabao (4)
Ubingwa Ngao ya Jamii (2)
UEFA Super Cup (1)
Kombe la Dunia la Klabu (1).
Makombe 4 msimu mmoja
Rekodi EPL pointi 100 (2017/18)