Guardiola awatolea uvivu wanaomshambulia
Muktasari:
- Man City ilishuhudia mabao 3-0 ugenini yakitinga katika nyavu zake na kukiacha kikosi hicho na mtihani wa kupambana mechi ijayo ili kufuzu hatua ya nane bora ya michuano hiyo.
MANCHESTER, ENGLAND: KIPIGO kinauma, wewe acha tu! Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amewajibu watu wanaomkosoa na kumshambulia baada ya kipigo cha mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya uliopigwa wiki hii dhidi ya Real Madrid.
Man City ilishuhudia mabao 3-0 ugenini yakitinga katika nyavu zake na kukiacha kikosi hicho na mtihani wa kupambana mechi ijayo ili kufuzu hatua ya nane bora ya michuano hiyo.
Hata hivyo, baada ya kipigo hicho wakosoaji wameongezeka katika mitandao ya kijamii wanaomshutumu kocha huyo kutokana na namna alivyopanga kikosi na pia jinsi ambavyo ‘sub’ zake zilishindwa kumbeba katika mchezo huo.
Lakini, Guardiola ni kama ameshindwa kuwavumilia watu hao, ambapo kabla ya mchezo wa ugenini wa Ligi Kuu England dhidi ya West Ham United alisema amechoshwa na kuwataka wamuache na kwamba kamwe hawezi kuvumilia waendelee kumfanya awafikirie wao.
Guardiola alitoa maelezo marefu akitetea uchaguzi wake wa kikosi, akisema wakosoaji mara nyingi humsifu anaposhinda, lakini humlaumu anapopoteza.
Kocha huyo alisema watu walimkosoa pia kabla ya mechi ya Newcastle United katika mechi ya Kombe la FA wiki iliyopita kwa kutowachezesha baadhi ya nyota kama Rodri na Bernardo Silva, huku akimuacha straika Erling Haaland nyumbani. Lakini, City walishinda 3-1, jambo lililowafanya wakosoaji haohao kubadili kauli na kuanza kusifia wachezaji.
Guardiola alisema: “Naitwa ‘genius’ tukishinda. Lakini tukipoteza, ghafla kila mtu ananishambulia. Nimefundisha mashindano haya kwa miaka 17, na kila ninapopoteza, ni kama ‘boom, pew, pew, pew’ - kila mtu ananishambulia.”
Guardiola pia alikumbuka uamuzi wake wa kumchezesha Ilkay Gundogan katika nafasi ya kiungo wa kati wakati City walipopoteza fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Chelsea 2021, akisema licha ya kwamba ulikuwa na sababu za kiufundi kulingana na hali ya wachezaji kama Rodri na Fernandinho wakati huo, lakini alipokea shutuma.
Pamoja na shutuma hizo aliwataka washambuliaji wake kuboresha viwango kwa kutumia vyema nafasi ndani ya boksi, hasa wakati Erling Haaland akipitia kipindi kigumu cha kutofunga mabao. Kabla ya jana, Haaland alikuwa amefunga mabao mawili kutokana na mchezo wa wazi katika mechi 17 zilizopita, na hakufanya makubwa dhidi ya Real Madrid.
Guardiola alisema: “Wachezaji waliopo ndani ya boksi wanapaswa kusogea vizuri zaidi kabla ya pasi kupigwa. Wanapaswa kuhisi mpira utaenda wapi.”
Hata hivyo, alisisitiza kuwa Haaland bado ni mshambuliaji bora duniani katika nafasi yake, lakini timu inahitaji kumsaidia zaidi kupata mabao.