Guardiola ampoza Grealish Man City
Muktasari:
- Grealish, 29, ndiye mchezaji ghari kwenye historia ya Ligi Kuu England, aliweka rekodi hiyo miaka minne iliyopita wakati alipohama kutoka Aston Villa kwa ada ya uhamisho ya Pauni 100 milioni.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola amemwomba radhi Jack Grealish kwa sababu hamchezeshi kiasi cha kutosha msimu huu.
Grealish, 29, ndiye mchezaji ghari kwenye historia ya Ligi Kuu England, aliweka rekodi hiyo miaka minne iliyopita wakati alipohama kutoka Aston Villa kwa ada ya uhamisho ya Pauni 100 milioni.
Staa huyo anayeweza kucheza nafasi karibu zote kwenye safu ya ushambuliaji alifanya vizuri chini ya Guardiola, 54, na alikuwa mtu muhimu kwenye kikosi cha Man City kilichonyakua mataji matatu ndani ya msimu mmoja, 2022-23.
Hata hivyo, mkali huyo wa kimataifa wa England ubora wake unaonekana kushuka kwa kipindi cha misimu miwili iliyopita, jambo lililomfanya aondoshwe pia kwenye kikosi cha England kilichocheza kwenye michuano ya 2024 kwenye majira ya kiangazi ya mwaka jana.
Grealish amefunga mabao mawili tu na asisti nne kwenye mechi 22 alizocheza kwenye michuano yote msimu huu, huku kwenye Ligi Kuu England amecheza dakika 604. Staa huyo wa zamani wa Aston Villa hajawekwa kwenye kikosi cha kwanza cha Guardiola tangu Januari 11, wakati Man City iliposhusha kichapo cha mabao 8-0 dhidi ya Salford City kwenye Kombe la FA.
Grealish alitarajia kupata nafasi nyingine ya kuichezea Man City kwenye mchezo wa raundi ya nne ya Kombe la FA dhidi ya Leyton Orient jana Jumamosi na kocha Guardiola alitazamiwa kutoa nafasi kwa wachezaji wengine.
Guardiola amemwomba msamaha Grealish hadharani, akisema ishu ya kukosa dakika nyingi za kucheza si kosa lake bali ni viwango vya Jeremy Doku na Savinho.
Guardiola alisema: "Nasema samahani kwa sababu hapati dakika anazostahili. Lakini, yote kwa yote ni juu ya mchango wa Jeremy na Savinho msimu huu, hiyo ndiyo sababu. Sio kwamba simpendi Jack au sina imani naye, lakini kubwa ni mchango wake ukilinganisha na wengine. Hiyo ndiyo sababu."