Guardiola ajitetea kiaina kuhusu Super League

LONDON, ENGLAND. KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola amesema kujiondoa kwao kwenye mashindano  ya European Supa Ligi  (ESL) ni ukurasa ambao umefungwa baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Aston Villa na kukaribia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England.

Manchester  City ni miongoni mwa klabu 12 ambazo zilionyesha nia ya kushiriki Ligi hiyo lakini kitendo cha kupigwa vita kuliwafanya kutangaza kujiondoa kwao Jumanne.

"Klabu imekubali kilichotokea na kujifunza lakini kwa sasa shabaha yetu ni kuangalia kwanini tupo hapa," alisema kocha huyo ambaye  timu yake inahitaji pointi nane tu kwenye michezo mitano iliyosalia ili kutangazwa kuwa mabingwa wa EPL.

"Ukurasa umeisha na umefungwa. Wamiliki hawana sababu ya kuomba msamaha kwangu, nawajua, najua vile walivyo," alisema kocha huyo ambaye ubingwa huo utakuwa wa tatu kwake ndani ya misimu minne akiwa na timu hiyo.

Ushindi wa mabao  2-1 ambao waliupata ugenini Manchester City dhidi ya Aston Villa, umewafanya kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa EPL kwa tofauti ya pointi 11 na Manchester United ambao wapo nafasi ya pili, Guardiola alisema ubingwa kwao, "Upo karibu mno."

Mabao ya Manchester City kwenye mchezo wa huo, yalifungwa na  Phil Foden na Rodrigo Hernández 'Rodri' huku la  Aston Villa likifungwa na John McGinn.