Guardiola aipiga mkwara FIFA

MANCHESTER, ENGLAND. KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola ameunga mkono tishio la Chama cha soka England (PFA) la kuishtaki Shirikisho la Soka duniani (Fifa) kutokana na kalenda yao yenye ratiba nyingi kuonekana inahatarisha afya za wachezaji.
Mkuu wa chama hicho, Maheta Molango alifichua wanachama wake wanataka kuchukua hatua za kisheria, baada ya mipango ya kuongeza mashindano mapya ya kimataifa, huku kukiwa na muda mchache wa mapumziko kwa wachezaji.
Guardiola alipendekeza mapema msimu huu wachezaji wanapaswa kufikiria kugoma, ili kuonyesha kutoridhika na ratiba nyingi za mechi.
Kocha huyo alisisitiza hajapendezwa na ratiba nyingi kubana kwenye kalenda ya Fifa, kwani wataathirika zaidi na ongezeko la mechi za Ligi ya Mabingwa na Kombe la Dunia la Klabu.
"Naelewa kabisa, alisema. "Ni wao tu wanaweza kubadilisha kitu (wachezaji). Nimezungumza sana, tuna mechi nyingi sana. Shida ni tuna wiki tatu tu za likizo katika msimu wa joto. Haitoshi kujiweka fiti. Angalia idadi ya majeruhi inaongezeka pia."
Kocha wa Aston Villa, Unai Emery aliwekea mkazo na kuiunga mkono PFA baada ya kauli ya Guardiola.
"Wachezaji wanacheza mechi nyingi sana, ngumu sana kwao. Kuna wengine wana nguvu ya kucheza, lakini wengine hawawezi. Tuna wachezaji wengi majeruhi, jambo ambalo sio la kawaida."
Wakati huo huo, Guardiola alikiri Jack Grealish alikuwa na wakati mgumu ndiyo maana akatolewa mapema kwenye ushindi wa mabapo 2-1 dhidi ya Sheffield United.
Grealish alishindwa kuendelea na mechi dakika ya sita tu kipindi cha pili, nafasi yake ikichukuliwa na Oscar Bobb.