Giannis ampora LeBron tuzo, Bucks ikibeba NBA

Muktasari:

  • Bucks imetokea nyuma kwa kufungwa mechi mbili za awali na kushinda mechi nne mfululizo kubeba taji hilo.

MIAKA 50 imetosha kwa timu ya Milwaukee Bucks, kubeba taji lao la pili la ligi ya kikapu Marekani (NBA).

Taji hilo limekuja kwenye mchezo wao wa sita wa fainali ya NBA, dhidi ya Phoenix Suns, wakiibuka na ushindi wa matokeo ya jumla 4-2.

Ushindi wa pointi 105-98 kwa Bucks, uliongozwa vema kabisa na staa wake Giannis Antetokounmpo, aliyefunga pointi 50 na kudaka ribaundi 14 kwenye mchezo wa sita uliowapa ubingwa wa NBA.

Giannis ambaye alikosekana kwenye mechi nyingi za msimu mrefu wa ligi (regular season), kutokana na majeraha, ameibeba timu yake kwenye fainali ambayo angeweza kukosa baadhi ya mechi.

Hatihati ya kutocheza baadhi ya mechi za fainali dhidi ya Suns, ilitokana na kuumia kwenye fainali ya Mashariki, Bucks waliposhinda dhidi ya Atlanta Hawks.

Giannis akisaidiwa vema na nyota wenzake akiwemo Khris Middleton na Jrue Holiday, walifanikiwa kuzima ubora wa Devin Booker na Chris Paul, walioing'arisha vilivyo timu ya Phoenix Suns.

Ubora wa Giannis kuibeba Bucks, umekuja na tuzo binafsi ya mchezaji mwenye thamani zaidi (MVP) wa fainali, akiichukulia mikononi mwa supastaa wa NBA, LeBron James.

LeBron ndiye alikuwa anaishikilia tuzo hiyo, aliyochukua kutokana na kuisaidia Los Angeles Lakers, kubeba taji hilo msimu uliopita mbele ya Miami Heat.