Gabriel Martinelli amwomba radhi Bradley
Muktasari:
- Bradley aliumia na kuanguka chini wakati wa mchezo wa Ligi Kuu England baina ya Arsenal na Liverpool usiku wa Alhamisi, ambapo kwa wakati huo ubao wa matokeo ya Emirates ulikuwa ukisomeka 0-0.
LONDON, ENGLAND: WINGA wa Arsenal, Gabriel Martinelli amemwomba radhi Conor Bradley kutokana na jaribio lake la kumsukuma beki huyo wa Liverpool ili atoke nje ya uwanja wakati alipokuwa ameumia.
Bradley aliumia na kuanguka chini wakati wa mchezo wa Ligi Kuu England baina ya Arsenal na Liverpool usiku wa Alhamisi, ambapo kwa wakati huo ubao wa matokeo ya Emirates ulikuwa ukisomeka 0-0.
Martinelli aliamua kumtoa beki huyo wa Liverpool ndani ya uwanja ili mchezo uendelee, kitu ambacho kimemtibua mchambuzi Gary Neville, akidai haikubaliki.
Bradley baadaye alibebwa kwa machela kutoka nje ya uwanja na aliondoka uwanjani Emirates akitembea kwa msaada wa magongo.
Martinelli alienda kuandika kwenye ukurasa wake wa Instagram: “Conor na mimi tumetumiana meseji na nimeshamwomba radhi. Sikuwa nimefahamu kama alikuwa siriazi kiasi hicho na kipindi kile mwili ulikuwa ushapata moto. Ninachotaka kusema, naomba radhi sana kwa kitendo kile. Namtakia Conor uponaji wa haraka.”
Martinelli alishinikizwa kuomba radhi na Neville, ambaye alikuwa mtangazaji mwenza wa mechi hiyo kupitia Sky Sports.
Neville amesema: “Huwezi kumsukuma mwenzako vile ili atoke nje ya uwanja. Hupaswi kufanya vile. Ile ni mbaya. Nadhani atahitaji kuomba radhi. Ona Bradley anatolewa kwa machela. Nimekasirishwa na Martinelli kusema ukweli. Nashangaa wachezaji wa Liverpool hawakwenda kwa nguvu kumvaa Martinelli!”
Daniel Sturridge na Roy Keane nao walimsema Martinelli kutokana na kitendo hicho.
Keane amesema: “Sio vizuri. Tunajua soka, mchezaji ni mtu mzuri. Kumrushia mpira, kumsimamia na kupiga goti ili kujaribu kumtoa nje, hiyo tabia nzuri nzuri. Nadhani Martinelli atalitazama hili na kuomba radhi, kwa sababu sio kitu kizuri.”
Sturridge aliongeza: “Hii inahuzunisha. Kuna ishu ya kutaka ushindi, kuna ishu ya kutaka kusaidia timu yako, lakini unapaswa kuwa na heshima kama mchezaji.” Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta alimtetea mchezaji wake akidai anamfahamu mchezaji wake kuwa ni mtu safi.