Gabriel Martinelli aandika rekodi mpya Arsenal
Muktasari:
- Nyota huyo wa Kibrazil, alifunga kwa shuti kali la mbali katika mchezo huo uliochezwa Jumatano usiku Desemba 10, 2025 nchini Ubelgiji, ikiwa ni mwendelezo wa kiwango chake bora kwenye michuano hiyo msimu huu.
Gabriel Martinelli ameweka rekodi mpya ndani ya klabu ya Arsenal baada ya kufunga bao muhimu katika ushindi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Club Brugge.
Nyota huyo wa Kibrazil, alifunga kwa shuti kali la mbali katika mchezo huo uliochezwa Jumatano usiku Desemba 10, 2025 nchini Ubelgiji, ikiwa ni mwendelezo wa kiwango chake bora kwenye michuano hiyo msimu huu.
Bao hilo lilikuwa la tano kwa Martinelli katika mechi tano mfululizo za Ligi ya Mabingwa, huku Arsenal ikipata ushindi wa 3-0, mabao mengine yakifungwa na Noni Madueke aliyetikisa nyavu mara mbili.
Kwa mafanikio hayo, Martinelli amekuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya Arsenal kufunga mechi tano mfululizo za Ligi ya Mabingwa Ulaya, rekodi ambayo hata gwiji Thierry Henry hakuwahi kuifikia.
Martinelli alianza kufunga dhidi ya Athletic Bilbao, Olympiakos, Atletico Madrid na Bayern Munich, kabla ya kuongeza lingine dhidi ya Brugge. Katika mchezo wa ufunguzi wa msimu dhidi ya Bilbao, alitoa pasi ya bao akitokea benchi, ingawa alilazimika kuikosa mechi ya Novemba 2025 dhidi ya Slavia Prague kutokana na majeraha.
Hadi sasa, kijana huyo mwenye umri wa miaka 24, ameongeza idadi yake ya mabao ya Ligi ya Mabingwa akiwa na Arsenal hadi kufikia tisa katika mechi 24.
Hata hivyo, Martinelli sasa ni mchezaji wa tatu katika historia ya Arsenal kufanikiwa kufunga mechi tano mfululizo katika michuano mikubwa ya Ulaya.
Ian Wright ndiye alikuwa wa kwanza kufanya hivyo katika michuano ya Cup Winners’ Cup msimu wa 1994-1995, akifunga katika mechi nane mfululizo na kuipeleka Arsenal hadi fainali, ingawa ilipoteza dhidi ya Real Zaragoza katika muda wa nyongeza.
Thierry Henry naye alifunga katika mechi sita mfululizo kwenye Kombe la UEFA msimu wa 1999-2000 chini ya Arsène Wenger, akianza dhidi ya Nantes katika hatua ya 32 bora hadi ushindi kwenye nusu fainali dhidi ya Lens. Hata hivyo, Arsenal ilipoteza fainali kwa penalti dhidi ya Galatasaray.
Sasa Martinelli ana nafasi ya kulingana rekodi na Henry endapo atafunga katika mechi inayofuata dhidi ya Inter Milan, Januari 20, 2026. Ili kufikia rekodi ya Wright, atalazimika kuendelea kufunga hadi hatua za mtoano.
Arsenal inatarajiwa kukamilisha hatua ya makundi kwa kuikaribisha Kairat kutoka Kazakhstan mwezi ujao, ikiwa hatua chache kufuzu moja kwa moja hadi hatua ya 16 bora baada ya kushinda mechi zote sita za mwanzo na kukusanya pointi 18.
Kocha Mikel Arteta ana matumaini kuwa kasi hii ya mabao ya Martinelli inaweza kuisukuma Arsenal hadi fainali ya Ligi ya Mabingwa na kuvunja mkosi wa kupoteza fainali za Ulaya.