Fury, Usyk kitapigwa Februari 27

LONDON. ENGLAND. IMETIKI. Lile pambano la wakali wawili wa masumbwi, Tyson Fury na Oleksandr Usyk la uzito wa juu (Heavyweight) kuwania mikanda minne (undisputed), rasmi sasa litafanyika Februari 27, Saudi Arabia.

Takriban miaka miongo miwili imepita bila kumpata bingwa wa mikando yote minne ya uzito wa juu na hili litakuwa la kwanza kuwaniwa mikanda hiyo na mabondia hao.

Kwa sasa Fury anashikilia mkanda wa WBC aliouchukua kutoka kwa Deontay Wilder, huku Usyk akiwa na mitatu ya WBO, WBA na IBF aliyoichukua kutoka kwa Anthony Joshua na atakayebeba yote atakuwa bingwa asiyepigika kutokana na rekodi za wote wawili.

Mabondia hao wanakutana wakiwa hawajapoteza mapambano yao, huku Usyk akionekana kujiamini zaidi atamchapa Tyson na kuchukua mikanda hiyo minne baada ya pambano la mwisho la Mwingereza huyo licha ya kushinda kwa pointi dhidi ya Francis Ngannou wengi wanaamini ameshuka kiwango.

Aliyekuwa bingwa wa mikanda ya IBF na WBC uzito wa Welterweight, Shawn Porter anaamini Fury atapoteza pambano hilo na anaweza akaomba lisogezwe mbele au lisewepo kutokana na kupungua makali yake.